Habari MsetoSiasa

Miondoko ya kipekee ya Ida Odinga akinengua kiuno

March 22nd, 2019 1 min read

Na CHARLES WASONGA

MKE wa kiongozi wa ODM Raila Odinga, Ida Odinga, na wabunge Gladys Wanga na Rosa Buyu ni maarufu kama ulingo wa siasa kando na kuwa watetezi sugu haki na kina mama na watoto wa kike.

Lakini katika video inayosambaa mitandaoni, viongozi hao wanaonekana wakionyesha weledi wao katika fani ya usakataji densi wakiwa Amerika.

Huku muziki wa Lingala wake msanii Moses Fanfan ukidunda, watatu hao wanaonekana wakionyesha miondoko kwa ustadi wa hali ya juu.

Huku wakiendana na muwala na mahadhi ya wimbo huo, watatu hao wanasikika walielekezana kuhusu staili ambayo wanafaa kuiga.

Viongozi hao ni miongoni wa wajumbe wanaohudhuru mkutano wa 63 kuhusu hadhi ya wanawake katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa (UN) jijini New York,  Amerika.

Mada ya mwaka huu ni “Mifumo ya Ulinzi wa Kijamii-Huduma za Umma na Miundo Mbinu kwa Usawa wa Kijinsia na Kuimarisha hali wa Wanawake na Wasichana.”

Kauli mbiu ni: Kuwapa Uwezo Wanawake na Uhusiano Wake kwa Maendeleo Endelevu.”

Mkutano huo ambao ulianza mnamo Machi 11, unatarajiwa kukamilika Ijumaa Machi 22.

Wanaohudhuria na wajumbe kutoka mataifa wanchama wa UN, mashirika ya UN na mashirika yasiyo ya kiserikali yanayofanya kazi kwa ushirikiano na Baraza la Umoja wa Mataifa kuhusu Masuala ya Kiuchumi na Kijamii (UNESCO).

Mkutano huo pia unahudhuriwa na Mama wa Taifa Bi Margaret na Gavana wa Kitui Charity Ngilu.