Habari Mseto

Mioto kwenye mbuga za kitaifa zatishia utalii

August 10th, 2020 2 min read

Na WINNIE ATIENO

WAWEKEZAJI katika sekta ya utalii wameitaka Wizara ya Utalii na Wanyamapori nchini kutangaza mikasa ya moto katika mbuga za kitaifa zilizo ukanda wa Pwani kama janga la kitaifa.

Kwa muda wa miezi mitatu sasa, mbuga za kitaifa eneo Pwani, zimekuwa zikikumbwa na mikasa ya moto mara kwa mara huku ikisababisha uharibifu mkubwa wa mamia ya ekari kwenye maeneo hayo.

Lakini wawekezaji wa sekta ya utalii na wanyamapori sasa wanamtaka waziri anayehusika na sekta hiyo, Bw Najib Balala kuanza uchunguzi wa mikasa hiyo wakilitaja kama janga hatari nchini.

“kulikuwa na mkasa wa moto katika mbuga ya Tsavo Magharibi usiku kucha kuamkia Jumamosi. Hatujawai kushuhudia uovu na uharibifu wa aina hiyo bila kuchukuliwa hatua na mamlaka ya kukomesha mikasa hiyo hatari. Bw Balala, hili sasa ni janga la kitaifa. Mikasa ya moto ya mara kwa mara inafaa kukomeshwa mara moja,” alisisitiza Bw Mohammed Hersi ambaye ni mtaalamu wa masuala ya utalii.

Bw Hersi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Shirikisho la Wadau wa Utalii nchini alisema awali mikasa hiyo ya moto ilianza kama ajali lakini baadaye ikachukua mkondo mpya.

Inashukiwa kuna watu ambao huanzisha moto kusudi mbugani kwa sababu ambazo hazijajulikana wazi.

Bw Hersi aliitahadharisha serikali akisema kuwa hatari inanukia kwenye mbuga hizo.

“Mwanzoni ilikuwa ni kama mikasa ya kawaida lakini namna mambo yanayoendelea tunakodolea hatari. Kila siku tunakumbana na janga la kuzima moto kwenye mbuga hizo. Uharibifu mkubwa unaendelea kutokana na mikasa ya moto. Hii si ajali,” akasema. Kama ni wafugaji wanahusika basi wanakosea maanake mifugo yao ikiwemo ngamia itakosa malisho,” alisema.

Kadhalika aliwaonya wakazi wanaoishi karibu na mbuga hizo kutoziharibu akisisitiza endapo wamejihusisha na mikasa hiyo basi huenda wakavamiwa na wanyama wa porini.

Mbuga ya Tsavo ina ndovu na vifaru wanaoishi humo ambao huenda wakaanza kuingia kwa maboma ya watu wakisaka malisho wakati tegemeo lao likiharibiwa.

Haya yanajiri siku chache baada ya Shirika La Wanyamapori nchini kuonya wakazi wanaopakana na mbuga hizo ikiwemo Tsavo na Chyulu dhidi ya kuwasha moto karibu na mbuga hizo.

Shirika hilo lilihusisha jamii jirani kwa mikasa hiyo.