Mipango kufanya Raila apate urais raundi ya kwanza

Mipango kufanya Raila apate urais raundi ya kwanza

Na MWANGI MUIRURI

IMEFICHUKA kuwa mrengo wa kisiasa wa Rais Uhuru Kenyatta unapanga njama fiche ya kumsaidia kinara wa ODM Raila Odinga kuibuka rais wa tano wa taifa hili baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka ujao kwa kumsaidia apate angalau asilimia 53 ya kura.

Katiba ya nchi hutoa sharti kuwa atakayeapishwa kuwa rais awe alishinda kwa zaidi ya asilimia 50.

Baada ya kufanya hesabu yao, washirikishi wa njama hiyo wanalenga kumsaidia Bw Odinga kutwaa kura zisizopungua 500, 000 kutoka Mlima Kenya, wazo ambalo limeshabikiwa na nduguye mkubwa Bw Oburu Odinga aliyesema kuwa “kwa muda huu wote urais ulikuwa ukimponyoka kwa kuwa hakuwa akipata usaidizi wa mitandao ya serikali iliyo mamlakani lakini safari hii tumepata hakikisho kuwa Baba hatahujumiwa.”

Akiwa na miaka 78 katika kura ya 2022, Bw Odinga akifanikiwa kushinda urais atakuwa ametimiza ndoto yake ya kuanzia 1982 alipokuwa na umri wa miaka 37 ambapo amekiri hadharani kuwa alijaribu kupindua serikali ya rais wa Pili marehemu Mzee Daniel Moi ili atwae uongozi wa nchi.

“Bw Odinga amekuwa akishindwa kuapishwa kama rais kupitia hujuma. Hila na njama kutoka kwa mabwanyenye wa Mlima Kenya pamoja na mitandao ya wanasiasa tajika wa eneo hilo ndizo zimekuwa zikimhangaisha Bw Odinga na kumpokonya ushindi mara kadha,” akasema aliyekuwa mbunge wa Maragua Bw Elias Mbau. Bw Mbau aliambia Taifa Leo kuwa kile kinahitajika kumsaidia Bw Odinga ni mabwanyenye hao waagizwe wasiingilie kumhujumu na hatimaye rais amuunge mkono kichinichini.

“Ikifanyika hivyo, Bw Odinga jinsi alivyokuwa akishinda lakini akaishia akahujumiwa, atafaulu wakati huu. Kile tunachohitaji sasa ni kumsaidia kura za Mlima Kenya zisiende zote kwa mwingine, afaulu tu kuvuna angalau asilimia 10 ya kura za eneo hilo zitakazopigwa,” akasema.

Jumapili iliyopita, aliyekuwa mbunge wa Gatanga na ambaye ndiye husemwa anaandaliwa kuwa mgombezi mwenza wa Bw Odinga alisema kuwa “mipango yote sasa inalenga kuhakikisha mwaniaji wa Mt Kenya ameorodheshwa katika urithi huo.”

Alisema kuwa njama inayoshirikishwa ni kuhusu nafasi ya Mlima Kenya katika serikali hiyo ya baada ya 2022 na akafichua kuwa Rais Kenuyatta ndiye atakuwa na usemi mkuu wa hisa za wenyeji katika mpangilio huo.

Bw Kenneth amekuwa akiandamana na Katibu Mkuu wa Muungano wa Wafanyakazi Nchini (COTU) Francis Atwoli, Seneta wa Siaya Bw James Orengo, Naibu Mwenyekiti wa Jubilee David Murathe, mwanasiasa wa Kaunti ndogo ya Kigumo Bw Kamau Mweha, Waziri wa Kilimo Bw Peter Munya na naibu kiranja wa wengi bungeni Bw Maoka Maore katika mikutano ya kuandaa uwaniaji wa Bw Odinga 2022.

Makuhani wakuu katika hali hiyo ni pamoja na Mbunge maalum Bw Maina Kamanda, aliyekuwa mbunge wa Dagoretti Kusini Dennis Waweru, Naibu wzairi wa Spoti Bw Zack Kinuthia, Mwenyekiti wa Baraza la Agikuyu (GCE) Bw Wachira Kiago na umoja wa muungano wa watu mashuhuri Mt Kenya na wengine.

Hata hivyo, wandani wa Naibu wa Rais Dkt William Ruto eneo la Mlima Kenya wamepuuzilia mbali njama hiyo wakiitaja kama itakayoaibishwa Mlima Kenya na kwingine.

“Ikiwa rais na washirika wake wanaenzi umoja wa taifa na demokrasia ya watu kujiamulia hatima yao ya kisiasa, wakome kuchokora mkondo wa 2022,” akasema Mbnge wa Gatundu Kusini Moses Kuria.

ambaye ni mbunge wa Gatundu Kusini akiongeza kuwa “Odinga na Mlima Kenya ni sawa na mafuta na maji ambayo hayawezi yakakubaliana kuchanganywa.

Mbunge wa Mathira Bw Rigathi Gachagua alisema kuwa “njama ya kuuza Bw Odinga Mlima Kenya ni ndoto chafu ambayo kamwe haitawahi kutimia.”

Aliambia Taifa Leo kuwa “Bw Odinga ni miongoni mwa majanga ya Mlima Kenya ambapo huhusishwa na uenezaji siasa za kutenga eneo hilo, kuzua mazingara hasi ya kibiashara kupitia mtindo wake wa kukataa matokeo ya chaguzi kupitia ghasia na pia tabia yake ya kujitafutia makuu kibinafsi na kuwaacha wengine wakingoja katika kingo za Mto Jordan yeye akiingia Kanani peke yake.”

Ni msimamo ambao unashikiliwa na Kinara wa Amani National Congress (ANC) Bw Musalia Mudavadi ambaye wiki jana akiwa katika kituo cha runinga cha Inooro alisema kuwa “Bw Odinga hawezi akawafaa kwa lolote watu wa Mlima Kenya au wa taifa hili kwa kuwa amejiangazia kama aliyejaliwa ubinafsi na hadaa.”

Bw Mudavadi alisema kuwa Bw Odinga hata hafai kuwania urais kwa kuwa alikuwa ametangaza kabla ya uchaguzi wa 2017 kuwa alikuwa amebakia tu na risasi moja ya kulenga urais kwa manufaa yake “lakini alipoambulia patupu, kwa sasa labda awe ameazima risasi nyingine, yake yaliisha na 2022 anafaa kuwa nje ya mchezo.”

You can share this post!

IEBC yasaka ardhi kuhamisha makao

Chama cha Ruto chaaibishwa uchaguzini Machakos