Habari Mseto

Miradi 'hewa' ya Jubilee kisiki kwa kampeni za Ruto

September 14th, 2019 2 min read

Na BENSON AMADALA

KUCHELEWESHWA kwa miradi mikuu ya serikali ya Jubilee katika Kaunti ya Kakamega, kumekuwa kizingiti kwa wandani wa Naibu Rais William Ruto kumpigia kampeni za 2022.

Wanasiasa wa Jubilee waliokutana na Dkt Ruto siku ya Jumatano ofisini mwake Nairobi, walieleza wasiwasi wao kuhusu utekelezaji duni wa miradi ya Jubilee ikiwemo uwekaji lami katika barabara za maeneo mbalimbali ya kaunti hiyo.

Duru za waliohudhuria mkutano huo zasema kuwa wandani hao pia walitaja kama kisiki matamshi ya baadhi ya wanasiasa wa Jubilee yanayoashiria kwamba wanavutiwa na muungano baina ya Dkt Ruto na kiongozi wa Amani National Congress (ANC) Musalia Mudavadi.

“Tumefanikiwa kuondoa jumbe za kuchanganya kutoka kwa mrengo wetu na sasa tuko tayari kumpigia debe Naibu Rais katika eneo hili,” alisema aliyekuwa Seneta wa Kakamega Dkt Boni Khalwale.

Mbunge wa Mumias Mashariki Bw Benjamin Washiali, ambaye pia ni mwandani mkuu wa Dkt Ruto katika Kaunti ya Kakamega, alisema kuwa kucheleweshwa kwa miradi ya Jubilee kunatia doa ahadi ambazo serikali iliwapa wakazi wa hapo ikiwemo uimarishaji wa miundo msingi.

Bw Washiali na wanasiasa wenzake Emmanuel Wangwe (Navakholo), Bernard Shinali (Ikolomani), Malulu Injendi (Malava), waziri wa zamani wa michezo Rashid Echesa, na Dkt Khalwale walisema barabara za eneo hilo ni mbovu sana na zinafaa kushughulikiwa.

“Tunataka Naibu Rais aingilie kati suala hili kwa sababu tumefanyiwa mzaha na wanakandarasi ambao hawana uwezo wa kukamilisha miradi. Ndiposa tunataka Naibu Rais atusaidie,” alisema Bw Washiali.

Vilevile, wanasiasa hao wanataka Dkt Ruto ashughulikie suala la kucheleweshwa kwa ujenzi wa taasisi za mafunzo ya kiufundi za maeneo bunge ya kaunti hiyo.

“Baadhi ya taasisi zimekamilika lakini wanakandarasi bado hawajazitoa kwa wasimamizi,” akalalama Bw Washiali.

Miradi kukamilika

Ahadi za maafisa wa serikali katika Kaunti ya Kakamega kwamba miradi mikuu itakamilishwa bila kuchelewa, hazijatimia na hilo limewakosesha wakazi matumaini. Moja ya miradi hiyo ni barabara ya Lurambi-Navakholo-Musikoma ya kilomita 31 katika eneobunge la Lurambi. Mradi huo ulizinduliwa na Rais Uhuru Kenyatta pamoja na naibu wake Dkt Ruto mwezi mmoja kabla ya uchaguzi mkuu wa 2017.

Lakini utekelezaji umekumbwa na hitilafu chungu nzima huku taarifa zikisema kuwa mwanakandarasi husika alijiondoa kwa kukosa uwezo wa kukamilisha ujenzi. Wakazi wamelalamika na hata kufanya maandamano baada ya mvua kubwa kusitisha usafiri kutokana na ubovu wa barabara.

Mbunge wa hapo Askofu Titus Khamala alieleza masikitiko yake jinsi mradi huo unavyoendeshwa.

Aliomba Waziri wa Usalama Dkt Fred Matiang’i kuingilia kati baada ya kuibuka kwamba mwanakandarasi huyo ameachana kabisa na mradi kwa sababu ya kukosa kupewa malipo ya kazi alizokamilisha.

“Tunataka serikali iingilie kati kuhakikisha wanakanadarasi wanafanya kazi zao ipasavyo ili mradi umalizike na kuletea wakazi manufaa,” akasema Askofu Khamala.

Katika kaunti ndogo ya Lugari, ujenzi wa barabara ya Soy-Seregea-Kilimani-Turbo ya Sh2.2 bilioni imefikia tu asilimia 3 kwa sasa.Barabara ya kilomita 12 ya Malava-Chebuyusi katika kaunti ndogo ya Kakamega bado haijaanza kujengwa.

Vilevile, mradi wa Sh500 milioni wa kuweka taa za mwangaza katika masoko ya kaunti bado haujaanza.