HabariSiasa

Miradi hewa yapunguza umaarufu wa Ruto

March 19th, 2019 1 min read

Na RUTH MBULA

UMAARUFU wa Naibu Rais William Ruto katika eneo la Kisii umeanza kushuka, kutokana na miradi iliyokwama na ahadi za maendeleo ambazo bado hazijatimizwa.

Wandani wake kutoka eneo hilo sasa wanadai wanakabiliwa vikali na wananchi kwa kutoa ahadi ambazo hazitimii.

Mnamo Ijumaa, walimwomba Dkt Ruto hadharani kuhakikisha kwamba miradi ambayo amekuwa akiwaahidi wakazi imekamilishwa, ili kuzima ghadhabu ambazo wanaelekezewa na wananchi.

Viongozi hao, ambao walikuwa wamehudhuria uzinduzi wa Maabara ya Hospitali ya Misheni ya Tabaka, walimpa Dkt Ruto orodha ya miradi yote ambayo aliahidi lakini haijakamilishwa.

Walimwambia Dkt Ruto kwamba wanakandarasi wanaoendesha baadhi ya miradi hiyo wanapaswa kubadilishwa ili kuharakisha kukamilishwa kwake.

Mwishoni mwa mwaka uliopita, Dkt Ruto alizuru kaunti za eneo hilo, katika kile kinachoonekana kama juhudi za mapema za kujitayarisha kwa kinyang’ayiro cha urais mnamo 2022.

Hata hivyo, kutokamilishwa kwa miradi hiyo kunahatarisha umaarufu wake katika eneo hilo lenye idadi kubwa ya wapiga kura.

Dkt Ruto amekuwa akiwaahidi wakazi mashine za kuhifadhi maziwa, ukarabati wa barabara, uimarishaji miundomsingi katika asasi mbalimbali kati ya ahadi nyingine.

“Mradi wa kuimarisha hospitali za Etago na Nduru, ambao ungegharimu Sh50 milioni ambao ulituahidi ungali kukamilika,” akasema kiongozi mmoja.

Naibu Gavana wa Kisii. Joash Maangi, wabunge Alpha Miruka (Bomachoge Chache), Sylvanus Osoro (Mugirango Kusini) na Prof Zadock Ogutu (Bomachoge Borabu) walisema nia yao ni kuona eneo hilo likistawi kimaendeleo kutokana na ushirika wao wa karibu na Dkt Ruto.

Kwa upande wake, Dkt Ruto amekuwa akitoa hakikisho kuwa miradi yote ambayo amekuwa akizindua itatekelezwa kwani ipo kwenye mipango ya serikali ya maendeleo.

Hata hivyo, wapinzani wake wamekuwa wakitumia kujikokota ama kukwama kwa miradi hiyo kumkabili kisiasa, wakisema alitoa ahadi hewa.