Makala

Miradi ya Daniel Moi

February 4th, 2020 3 min read

Na CHARLES WASONGA

RAIS mstaafu Daniel Moi ambaye amefariki mapema Jumanne, wakati wa uhai wake alianzisha miradi mbalimbali ambayo inaakisi kumbukumbu ya utawala wake wa miaka 24.

Mojawapo ya miradi hiyo ni mfumo wa sasa wa elimu wa 8-4-4 ulioanishwa mnamo mwaka wa 1985 ambapo mwanafunzi anasoma kwa miaka minane katika shule ya msingi, miaka minne katika shule ya upili na miaka minne katika chuo kikuu au vyuo vya kadri.

Mfumo huu, ambao serikali inapanga kuufutilia mbali, ulichukua mahala pa mfumo wa zamani wa 7-4-2-3. Chini ya mfumo huu mwanafunzi alisoma kwa miaka saba katika shule ya msingi, kisha miaka nne katika kiwango cha chini ya shule ya upili (O-Level), kisha anajiunga na kidato cha tano na sita (maarufu kama A-Level) na miaka mitatu katika chuo kikuu.

Kimsingi, mfumo wa 8-4-4 ulianzisha masomo ya kiufundi kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha nne lengo likiwa ni kumpa mwanafunzi ujuzi ya kumwezesha kujitegemea maishani baada ya kufanya mtihani wa kitaifa wa darasa la nane (KCPE) na ule wa kidato cha nne (KCSE).

Watoto walifunzwa masomo kama vile; useremala, ushonaji nguo, uashi, muziki, sanaa ya uchoraji miongoni mwa masomo mengine ya kiufundi.

Lakini baada ya miaka kadhaa serikali ilianza kuonyesha dalili za kushindwa kufikia malengo asilia ya mfumo huu kwani ilishindwa kufadhili ujenzi wa karakana za kuendeshea masomo ya kiunfundi katika shule zote za umma.

Hatimaye katika miaka ya 1990s serikali iliifanyia mageuzi mfumo huo wa elimu kwa kuondoa masomo ya kiufundi kwenye orodha ya masomo ya lazima ya kutahiniwa katika mitihani ya KCPE na KCSE. Hata hivyo, masomo hayo yameendelea kufundishwa katika vyuo vikuu, vyuo vya kadri na vyuo anuwai.

Ni baada ya serikali ya sasa kung’amua kuwa mfumo wa 8-4-4 umekuwa ukizingatia zaidi uwezo wa mwanafunzi kupita mitihani ya kitaifa na kukosa umilisi wa masomo aliofundishwa ndipo ikaamua kuanzisha mfumo mpya wa elimu wa 2-6-3-3-3.

Chini ya mfumo huu mtoto atasoma kwa miaka miwili katika shule ya chekechea, miaka sita katika shule ya msingi, miaka mitatu katika daraja la chini la shule ya upili, miaka mitatu katika daraja la juu shule za upili na miaka mitatu katika vyuo vikuu.

Lakini akiongea katika shule ya upili ya Sunshine, Nairobi mnamo 2016 Mzee Moi alipinga kuondolewa kwa mfumo wa 8-4-4 akisema wale waliopitia mfumo huu wameng’aa kimasomo katika mataifa ya ng’ambo kama vile Amerika, Japan, na Uingereza.

“Isitoshe, kizazi cha sasa cha viongozi na wataalamu walipitia mfumo wa 8-4-4 na utendakazi wao umekuwa wa kupigiwa mfano,” akasema.

Mabasi ya Nyayo

Mabasi ya Uchukuzi ya Nyayo (NBS) yalianzishwa na Rais mstaafu Daniel Moi mnamo 1986 kwa lengo la kutoa huduma za uchukuzi jijini Nairobi. Mwanzoni, idadi ya mabasi yaliyozinduliwa ilikuwa 20.

Sababu ni kwamba serikali ilidai mabasi ya kampuni ya Kenya Bus Services (KBS) yalilemewa na ongezeko la idadi ya watu jijini nyakati hizo.

Lakini wakosaoji wa mpango huo walidai kuwa serikali alianzisha mabasi ya Nyayo kwa sababu ilitaka kudumaza kampuni ya KBS iliyoingia nchini mnamo 1934 ikiitwa Oversees Transport Company (OTC) baada ya kampuni hiyo ya Uingereza kukataa kuiuzia sehemu za hisa zake.

Mabasi hayo, ya rangi ya kijani kibichi yalikuwa yakitoza nauli nafuu kuliko mabasi ya KBS na wahudumu wake walitoka Shirika la Vijana kwa Huduma ya Taifa (NYS).

Kwa hivyo, mabasi hayo yalipendwa na wananchini kiasi kwamba miaka miwili baadaye, mnamo 1988, idadi ya mabasi hayo iliongezeka hadi 89. Iliingiza faida ya Sh9 milioni katika kipindi hicho cha miaka miwili kulingana na ripoti za vyombo vya habari zilizomnukuu mkurugenzi mkuu wa kampuni hiyo wakati huo Geoffrey Griffins.

Na katika miaka ya 1990s idadi ya mabasi ya NBS iliongezeka hadi zaidi ya 300 na huduma zake zikasambazwa kutoka Nairobi hadi maeneo mengine ya nchini.

Lakini kuanzia mwaka wa 1994, kutokana na usimamizi mbaya na ufisadi miongoni mwa wafanyakazi na wasimamizi wa mabasi hayo, kampuni hiyo ilianzia kufifia.

Mnamo Julai 1994 iliripotiwa kuwa kati ya mabasi 367 ambayo yalikuwa yakihudumu kote nchini ni mabasi 55 pekee ilikuwa imesalia barabarani huku mengine yakiwa yamekwama.

Hatimaye mnamo 1997 kampuni hiyo ilisitisha shughuli na mamia ya Wakenya kutoka NYS na vyuo vikuu wakaachwa bila ajira.

Siku hizi baadhi ya mabasi hayo, ambayo yamechakaa, yameagezwa katika karakana ya NYS eneo la Ruaraka. Mnamo 2004 serikali iliunza baada ya mabasi hayo, kuwa njia ya mnada.

Mwaka 2018 serikali ya Jubilee ilijaribu kuanzisha upya huduma za mabasi hayo jijini Nairobi lakini kwa kuzindua mabasi 27 lakini mpango huo umegonga mwamba.

Mabasi hayo yalikuwa yakihudumu katika ruti za mitaa ya Kibera, Githurai, Mwiki, Kariobangi, Mukuru Kwa Njenga, Dandora na Kawangware na katikati mwa jiji huku yakitoza nauli ya Sh20 pekee.

Hata hivyo mabasi hayo yamekuwa mara kwa mara yakisitisha huduma kutokana na kile kilichotajwa kama “kupanda kwa gharama ya utunzaji na huduma nyinginezo”.