Miradi ya handisheki yakimbizwa ikamilike

Miradi ya handisheki yakimbizwa ikamilike

NA WAANDISHI WETU

PUNDE tu baada ya handisheki kati ya Rais Uhuru Kenyata na mpinzani wake mkuu kwenye uchaguzi mkuu wa 2017, Raila Odinga, serikali ya kitaifa ilitekeleza miradi kadhaa ya maendeleo katika ngome ya kiongozi huyo wa upinzani.

Hii ilisaidia kiongozi huyo wa ODM kuonyesha wafuasi wake kwamba hatua hiyo ilikuwa ya kujali maslahi yao.

Lakini sasa muda unasonga kuelekea mwisho wa utawala wa Rais Kenyatta huku juhudi zikifanywa kuharakisha miradi hiyo ikamilike kabla ya Agosti 9.

Katika Kaunti ya Kisumu, miradi hiyo imebadilisha sura ya kaunti hiyo iliyo kando mwa Ziwa Victoria.

Bw Odinga na kiongozi wa nchi wanatarajiwa kutumia miradi hiyo ya mabilioni ya pesa kurai eneo la Magharibi kwa ahadi litanufaika na maendeleo zaidi iwapo kinara huyo wa upinzani ataingia ikulu.

Wiki mbili zilizopita, maafisa wa serikali ya kitaifa wakiongozwa na Msemaji wa Serikali Kanali Mstaafu Cyrus Oguna, walitembelea miradi hiyo na kukagua jinsi inavyoendelea kutekelezwa.

Kamishna wa Kaunti ya Kisumu Josephine Ouko, ambaye ni mwenyekiti wa Kamati ya Utekelezaji wa Maendeleo katika kaunti hiyo alisema asilimia 100 ya mingi ya miradi hiyo imekamilika.

“Mingi ya miradi iko tayari. Tumekuwa tukiwaharakisha wanakandarasi. Mashine zinaendelea kufanya kazi na wanajaribu kuhakikisha imekamilishwa kwa wakati,” alisema Bi Ouko.

Baadhi ya miradi ambayo tayari imekamilishwa ni bandari ya Kisumu ambayo ilikarabatiwa kwa gharama ya Sh3 bilioni, chuo cha Railway Training Institute Marine School kilichogharimu Sh476 milioni na kampuni ya kutengeneza meli ya Kisumu Ship Yard.

Kuanza kutumiwa kwa Bandari ya Kisumu kunatarajiwa kupigwa jeki na ujenzi wa meli mpya ya mizigo ya MV Uhuru II ambayo kufikia sasa asilimia 60 imekamilika na inatarajiwa kukamilishwa kabla ya Agosti 2022.

Kulingana na Shirika la Reli la Kenya na Mamlaka ya Bandari Kenya (KPA), MV Uhuru II, itakuwa na uwezo wa kubeba tani 1,800 ikiwa ni tani 540 zaidi ya inazobeba MV Uhuru I.

Mradi mingine ambayo imekamilishwa ni ukarabati wa reli ya kilomita 216 kutoka Nakuru hadi Kisumu ambayo mwaka jana ilianza kusafirisha abiria na pia ilifanyiwa majaribio ya kubeba mizigo na Uhuru Business Park.

Barabara ya pande mbili ya kilomita nne iliyogharimu Sh2.8 bilioni ya Mamboleo iko karibu kukamilika sawa na ile ya Mamboleo Interchange huku ujenzi wa barabara ya kilomita 62 ya Mamboleo-Kipsitet Muhoroni ikianza kutoka upande wa Muhoroni.

Handisheki pia ilipeleka miradi miwili ya barabara kaunti ya Siaya; ya kilomita 12 kutoka Got Nanga—Bar Ober kaunti ndogo ya Ugenya na ya kilomita 27 kutoka Bondo—Uyawi—Liunda kaunti ndogo ya Bondo.

Ripoti za Kassim Adinasi, Benson Amadala, Ruth Mbula, Rushdie Oudia, Derick Luvega na George Odiwuor

You can share this post!

Burnley wazidisha masaibu ya kocha Antonio Conte kambini...

TUSIJE TUKASAHAU: Serikali ina mazoea ya kutenga mabilioni...

T L