Miriam Osimbo: Nimejiwekea malengo ya kumiliki brandi ya filamu

Miriam Osimbo: Nimejiwekea malengo ya kumiliki brandi ya filamu

NA JOHN KIMWERE

NI miaka 14 sasa tangia ajitose kwenye ulingo wa uigizaji ambapo anajivunia kwa kati ya wasanii wanaozidi kuvumisha tasnia ya maigizo nchini.

Anashikilia kuwa ingawa miaka iliyopita wengi walikuwa na kasumba ya kwamba usanii ni uhuni miaka ya sasa wengi wanaume kwa wanawake wamekumbatia uigizaji maana wametambua ni ajira kama nyingine.

Kando na uigizaji ni msanii wa injili ambaye pia aliwahi kuwa mtangazaji kwenye redio ya Mulembe FM. Miriam Osimbo Oluoch ama ukipenda Nanjala Actress anadokeza kuwa marehemu mamake aliyekuwa mwalimu alichochea kipaji chake pakubwa.

Ingawa hajafikia malengo yake anasema kamwe hawezi kujutia kujitosa katika uigizaji maana mapato yake yamemsaidia pakubwa kugharamia mahitaji muhimu kimaisha ikiwamo kuleta mkate mezani, kumvisha pia kulipa kodi ya nyumba.

”Nilipata motisha zaidi kushiriki filamu nilipotazama msanii Mhonja kwenye filamu ya Tausi iliyokuwa inapeperushwa kupitia runinga ya KBC,” amesema na kuongeza kuwa amepania kuibuka produsa pia kumiliki brandi yake ili kukuza talanta za waigizaji wanaoibukia. Katika mpango mzima amepania kufuata nyayo za waigizaji wa filamu za Kinigeria (Nollywood), Genevieve Nnaji na Mercy Johnson. Genevieve Nnaji anajivunia kufanya kazi nzuri kama ‘Blood Sister,’ na ‘Power of Love,’ kati ya nyingine.

Naye Mercy Johnson ameshiriki filamu nyingi tu zikiwamo ‘Heart of a Fighter’, ‘The Maid’ na ‘Weeping Soul’ miongoni mwa nyingine.

Dada huyu aliyezaliwa mwaka 1989 alianza kupiga shughuli chini ya kundi la Jicho Four Production na Planet Theater Production kuzalisha filamu kupitia mwongozo wa vitabu za riwaya (setbooks).

Baadaye alianza kukwea ngazi ambapo alijiunga na kampuni ya Al Li Son Production na kushiriki filamu ya Siri Drama iliyopeperushwa kupitia Citizen TV.

Kwa jumla dada huyu ameshiriki filamu kama ‘Hulabaloo Estate’, ‘Vioja Mahakamani’, ‘Inspekta Mwala’, ‘Mashtaka’, ‘Nairobi Law’,’Sky Girls’ na ‘Siri Drama’ kati ya nyingi nyinginezo.

Miriam Osimbo Oluoch ama ukipenda Nanjala Actress anadokeza kuwa marehemu mamake aliyekuwa mwalimu alichochea kipaji chake pakubwa. PICHA | JOHN KIMWERE

Kwenye vipindi vya Vioja Mahakamani na Hulabaloo Estate alishiriki kama mke wa Makokha ambazo zimepata kuonyeshwa kupitia KBC TV na Maisha Magic East mtawalia.

Akiwa mtangazaji kati ya mwaka 2012 na 2016 alikuwa wakisukuma gurudumu ya kipindi cha Bhukha Bushire akishirikiana na watangazaji wenzie Sumba Juma na Omar Bakuli.

Kwa kipindi hicho amekuwa katika sekta ya uigizaji anasema amejifunza mengi ambapo kamwe sio mchoyo wa mawaidha. Anawaambia wanawake wenzie kuwa wajiamini, wajiheshimu pia wafanye wanachopenda tena kwa kujitolea bila kujishusha hadhi. Wakipata nafasi waonyeshe uwezo wao kana kwamba hakuna kesho, maana endapo sio sasa ni sasa hivi. Aidha anawahimiza kuwa hauwezi kutumia fimbo ya mbali kuumua nyoka ambapo ni vyema kutumia talanta waliotunukiwa kusaka riziki bila kutarajia baraka wasiofahamu itashuka lini.

”Hakika kuwa katika sekta ya uigizaji kwa kipindi hicho sio jambo rahisi nimesoma mengi,” akanena.

Kwa waigizaji wa humu nchini analenga kutinga hadhi yake msanii wa kimataifa Mkenya, Lupita Nyong’o. Pia angependa kufanya kazi na waigizaji kama Awinja (aliyekuwa akishiriki kipindi cha Papa Shirandula) na Sanaipei Tande.

”Tatizo la sekta ya filamu hapa nchini ni malipo duni jambo linalofanya wengi wetu kutopiga hatua yoyote maishani,” akasema.

Anataka serikali iweke mikakati kabambe kuhakisha wasanii wanalipwa vizuri ili kupaisha tasnia hiyo. Kuhusu masuala ya mapenzi anasema hawezi kuweka katika kaburi la sahau aliwahi kulia alipogundua wakati wowote alipokuwa akitoa hela kumpiga jeki mpenzi wake naye alikuwa akizitumia kusaidia mpenziwe wa kike.

  • Tags

You can share this post!

Mahujaji 3,000 kusafiri Mecca, Covid ikifungia wengine

KINYANG’ANYIRO 2022: Pokot Magharibi

T L