Habari MsetoSiasa

Mishi Mboko kujengea wasichana shule

February 27th, 2019 1 min read

NA HAMISI NGOWA

MBUNGE wa Likoni, Bi Mishi Mboko amewahimiza wazazi katika eneobunge hilo waache mila zinazowanyima nafasi ya elimu watoto wa kike.

Bi Mboko alisema hali ya maisha kwa sasa imebadilika kinyume na ilivyokuwa awali ambapo ajira kama zile za kujiunga na jeshi na vikosi vingine vya usalama, zilikuwa zikitafutiwa vijana wa kiume.

“Nakumbuka enzi za utotoni, kazi kama zile za jeshi na hata polisi zilikuwa zikiwatafuta majumbani bila ya kuhitaji vyeti vya elimu. Lakini nyakati hizo haziko tena. Kazi hakuna na zile kidogo zinazopatikana lazima uwe na stakabadhi,” akasema.

Alisema yeye kama mbunge amejitolea kuhakikisha kuwa eneo hilo linakuwa na shule za umma za kutosha ili kutoa nafasi kwa watoto wote kupata elimu.

Mbunge huyo ambaye alikuwa akizungumza katika eneo la Shika Adabu wakati wa kuweka jiwe la msingi la shule ya upili ya malazi ya wasichana ya Mishi Mboko Girls, alidokeza kuwa azma yake ni kujenga shule zaidi za upili na msingi ili kupunguza msongamano wa wanafunzi shuleni.

Alieleza kuwa kwa sasa eneo hilo linashuhudia msongamano mkubwa wa wanafunzi katika shule za msingi na upili kutokana na upungufu uliopo wa shule za umma katika eneo hilo.