Misimamo mikali yazuia majadiliano ya RaiRuto

Misimamo mikali yazuia majadiliano ya RaiRuto

CHARLES WASONGA Na WANDERI KAMAU

MISIMAMO mikali ya wanasiasa wa mirengo ya Kenya Kwanza na Azimio la Umoja-One Kenya ndio imekwamisha juhudi za kupatanisha Rais William Ruto na Raila Odinga ili kuzuia maandamano ya Jumatatu.

Katika siku za hivi karibuni, viongozi wa kidini na wanachama wa vyama vya wataalamu mbalimbali nchini wamekuwa kwenye mstari wa mbele kumshinikiza Rais Ruto kufanya mazungumzo na Bw Odinga wakisema maandamano yatavuruga amani na uchumi wa nchi.

Lakini viongozi kadhaa katika kambi ya Rais Ruto, wakiongozwa na Naibu wake Rigathi Gachagua, kiongozi wa wengi katika Bunge la Kitaifa Kimani Ichung’wa, mwenzake wa Seneti Aaron Cheruiyot wamepuuzilia mbali miito hiyo.

Wanashikilia kuwa Rais Ruto hapaswi kufanya mazungumzo yoyote na Bw Odinga wanayedai anataka kuchochea vurugu nchini ili “aingie serikalini kupitia handisheki”.

Akiongea Ijumaa kwenye mahojiano katika vituo vya redio vinavyotangaza kwa lugha ya Agikuyu, Bw Gachagua alisisitiza kuwa, Rais Ruto hafai kufanya mazungumzo na Bw Odinga kwani ana historia ya kuvuruga serikali za marais wa zamani.

“Huyu ni mtu ambaye tunajua historia yake ya kusambaratisha serikali zilizochaguliwa. Alimsumbua Uhuru mpaka akafaulu kuingia katika serikali kupitia handisheki. Vile vile, alisumbua marais Mwai Kibaki na Daniel Moi kupitia maandaamano kama haya. Nataka kumwambia kuwa nikiwa ndani ya serikali hii ya William Ruto asahau handisheki kabisa,” akasema.

Akaongeza: “Watoto wa Raila na Kalonzo Musyoka (kiongozi wa Wiper) wako katika Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EALA), kule Tanzania. Wasiwapotoshe Wakenya na kuwatumia watoto kufanya maandamano. Tunamjua yule anayemfadhili. Raila hana mamlaka yoyote kuitisha au kutangaza siku ya mapumziko Jumatatu.”

Bw Gachagua alisema mazungumzo ya kipekee ambayo serikali inaweza kufanya na Odinga ni namna atakavyostaafu siasa na kuelekea nyumbani kwake Bondo.

“Tunawarai watu wetu kuendelea na shughuli zao kama kawaida Jumatatu bila uoga wowote,” akaeleza.

Na kwenye kikao na wanahabari katika majengo ya Bunge, Alhamisi wiki hii Bw Ichung’wa aliwaaongoza wabunge 20 wa Kenya Kwanza kushikilia kuwa Rais Ruto hawezi kufanya mazungumzo na Bw Odinga wakidai anapanga mapinduzi ya serikali “iliyochaguliwa kidemokrasia,”

“Rais Ruto hana wakati wa kuzungumza na mtu kama Raila ambaye anapania kutenda kosa la uhaini kupitia maandamano kinyume cha sheria. Wakenya wamemtwika jukumu la kuwafanyia kazi,” akasema.

“Serikali zilizopita huenda zilimfanya Raila kuhisi kwamba yuko juu ya sheria. Lakini tuko hapa kuhakikisha kuwa sheria inamwandama. Vurugu zozote zikitokea Jumatatu, yeye ndiye atawajibika,” mbunge huyo wa Kikuyu akasema na kuungwa makono na kiranja wa wengi Silvanus Osoro.

Wanasiasa wengine wa mrengo wa Kenya Kwanza ambao wamemhimiza Rais Ruto kumpuuzilia mbali Bw Odinga ni pamoja na kiongozi wa wachache katika Seneti Aaron Cheruiyot, Samson Cherargei (Seneta Nandi), George Murugara (Mbunge wa Kiambu), John Kaguchia (Mukurweini), miongoni mwa wengine.

Katika mrengo wa Azimio, kundi la wenye msimamo mkali linaongozwa na kiongozi wa wachache katika bunge la kitaifa Opiyo Wandayi, Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna, Ledama Olekina (seneta wa Nairobi), miongoni mwa wengine.

“Tunataka kuwatangazia Wakenya wote kwamba, maandamano ya Jumatatu jijini Nairobi yataendelea yalivyopangwa. Hakuna chochote ambacho kitatuzuia kukongamana jijini Nairobi ili kudai kile ambacho ni haki yetu,” Bw Wandayi akasema kwenye kikao na wanahabari Alhamisi katika majengo ya Bunge.

Kwa upande wake, Bw Sifuna alisema wafuasi wa Azimio wana haki ya kikatiba kufanya maandamano popote nchini na wafuasi wa Kenya Kwanza hawana mamlaka ya kuibua pingamizi zozote.

“Tuliupa huu utawala wa Ruto muda wa siku 14 kushughulikia matakwa yetu yakiwemo kupunguzwa kwa gharama ya maisha na kufunguliwa kwa sava za IEBC. Lakini kufikia sasa kile ambacho wamekuwa wakifanya ni kujipiga vifua. Sasa Jumatatu Wakenya wataitisha haki yao,” akasema Katibu huyo mkuu wa ODM.

Mapema wiki hii, viongozi wa kidini walimtaka Rais Ruto kuonyesha sifa za uongozi kwa kufanya mazungumzo na viongozi wa upinzani kwa manufaa ya nchi.

Aidha, walimtaka Bw Odinga kufutilia mbali maandamano ya Jumatatu na akumbatie mazungumzo.

“Viongozi wa kisiasa wakiongozwa na Rais Ruto na kiongozi wa Azimio Bw Odinga wakomeshe vitendo na matamshi yanayoweza kusababisha machafuko. Wawili hawa waketi pamoja na wazungumze ili kuondoa taharuki nchini; mazungumzo sio handisheki,” akasema Askofu Martin Kivuva wa Kanisa Katoliki jimbo la Mombasa.

  • Tags

You can share this post!

Jopo la IEBC latoa hakikisho la kuteua mwenyekiti kwa njia...

Tanzia: Mwanamume amuua nduguye kabla kujitia kitanzi

T L