Habari Mseto

Misongamano mijini wananchi wakielekea mashambani kwa Krismasi

December 24th, 2020 2 min read

Na FRANCIS NDERITU

MISONGAMANO mikubwa ya watu ilishuhudiwa jana katika vituo vya magari jijini wakazi wakielekea maeneo mbalimbali kwa sherehe za Krismasi.

Abiria waliokuwa wakielekea Meru, Isiolo na maeneo ya Magharibi walikuwa wamekwama kwenye vituo vya matatu, huku waking’ang’ania magari machache yaliyopatikana.

Wahudumu nao walitumia fursa hiyo kupandisha nauli.Uchunguzi wa Taifa Leo katika vituo mbalimbali vya magari jijini Nairobi ulionyesha umati mkubwa wa wasafiri wakiwa wamekaa nje kwenye jua wakisubiri magari.

Katika kampuni ya mabasi ya Kensilver iliyo kwenye barabara ya Dubois ambayo huhudumu kati ya Nairobi na Meru, abiria walikuwa wamesongamana.

Baadhi walikalia mizigo yao wakisubiri gari.Hali ilikuwa sawa na hiyo kwenye barabara ya Accra ambako kunapatikana matatu zinazosafiri kuelekea maeneo ya Mlima Kenya kama vile Nyeri, Karatina, Mwea na Embu.

Waliozungumza na Taifa Leo, walisema walikuwa tayari kusubiri hadi pale watakapopata magari ili waende kusherehekea sikukuu ya Krismasi na jamaa zao mashambani.

Wengine walisema hawajali kama watalipishwa kiasi gani cha nauli, mradi tu wapate nafasi kwenye magari hayo.Meneja wa Sasa Line, Bw Ali Otieno alisema abiria walikuwa wengi kuliko idadi ya magari waliyo nayo.

“Abiria ni wengi na hatuna magari ya kutosha. Isitoshe, uhaba huu pia unachangiwa na kanuni za Wizara ya Afya kudhibiti kusambaa kwa corona. Inatulazimu tubebe idadi inayotakikana,” akasema.

Kwenye kituo cha matatu hizo, abiria walionekana wakinawa mikono na kuvalia maski kabla ya kuingia kwenye magari.Kutokana na kanuni hizo ambapo kwa mfano gari la abiria 14 linalazimika kubeba wanane pekee, wenye magari katika vituo vyote ambavyo Taifa Leo ilipitia walikuwa wameongeza nauli kufidia viti vilivyokosa kukaliwa.

Katika barabara ya Mfangano, vituo vya matatu za North Rift Shuttle na Great Rift Express Shuttle vilifurika abiria kufikia saa mbili asubuhi.

Kulingana na usimamizi wa kampuni hizo mbili ambazo matatu zao huhudumu Eldoret, Kitale na Bungoma, uhaba wa abiria wanaosafiri kwenda Nairobi ndio sababu ya kuongezwa kwa nauli.