Michezo

Misri yaipiga Tanzania 1-0 kirafiki

June 14th, 2019 2 min read

Na GEOFFREY ANENE

BAO la Ahmed Elmohamady katika dakika ya 64 lilisaidia Misri kuzamisha Taifa Stars ya Tanzania 1-0 katika mechi ya kirafiki kabla ya kumenyana na Harambee Stars ya Kenya, Teranga Lions ya Senegal na Desert Warriors ya Algeria katika mechi za Kundi C kwenye Kombe la Afrika (AFCON) jijini Cairo.

Mafirauni wa Misri, ambao ushindi huu ni wao wa sita bila kuandikisha sare ama kupoteza dhidi ya Tanzania, walitawala mechi kutoka kipenga cha mwanzo wakitafuta bao la mapema.

Kipa Aishi Manula alihakikisha Tanzania inaingia mapumzikoni 0-0 baada ya kupangua makombora kutoka kwa Amr Warda dakika ya sita na 22, kichwa cha Ayman Ashraf dakika ya 34 na shuti la nahodha Elmohamady dakika za mwishomwisho za kipindi cha kwanza lililoondolewa kwenye laini ya goli na beki Gadiel Kamagi.

Dakika tano baada ya kipindi cha pili kuanza, Walid Soliman alipiga mpira wa kichwa kwenye mwamba alipopokea krosi murwa kutoka kwa Elmohamady.

Krosi ya Ahmed Mansour kutoka pembeni kushoto dakika ya 64 ilimpata Elmohamady vyema na akaikamilisha kwa ustadi hadi wavuni kupitia kichwa chake.

Tanzania karibu isawazishe dakika za lala-salama pale nahodha Mbwana Samatta alipata mpira katikati ya uwanja na kufanya shambulizi katika lango la Misri, lakini kipa Mahmoud Abdelrahim almaarufu ‘Gennesh’ alikuwa macho kupangua kiki lake.

Mechi ngumu

Baada ya mechi, Samatta aliambia Shirikisho la Soka la Tanzania (TFF) kwamba ilikuwa mechi ngumu, lakini nzuri itakayowezesha benchi la kiufundi kutambua makosa na kuyarekebisha kabla ya mechi ijayo ambayo ni ya kirafiki dhidi ya Zimbabwe hapo Juni 16.

Aliongeza, “Ugumu wa kucheza na Misri ndio ugumu tutakaopata katika mechi zetu za makundi katika Kombe la Afrika kwa hivyo ni mchuano ambao umekuwa mtihani mzuri kwetu.”

Kocha Emanuel Amunike alikiri pia Tanzania ilipimana nguvu dhidi ya timu nzuri na kali sana. “Ni mafunzo mazuri tumepata na yatatusaidia kurekebisha makosa kabla ya mechi zetu zijazo,” raia huyo wa Nigeria aliongeza.

Misri itakamilisha mechi zake za kirafiki dhidi ya Guinea mnamo Juni 16. Kwenye kipute cha AFCON, ambacho kitaanza Juni 21 na kutamatika Julai 19, Misri italimana na DR Congo, Uganda na Zimbabwe katika mechi za Kundi A.