Michezo

Miss BumBum kutumia chambo tofauti kunasa penzi la Messi

May 20th, 2019 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

MSHINDI wa zamani wa taji la Miss BumBum, Suzy Cortez amezidi kudhihirisha ukubwa wa penzi lake kwa nyota Lionel Messi kwa kuchanja chale nyinginezo za kudumu kwenye sehemu za ndani ya mapaja yake.

Suzy ambaye ni shabiki mkubwa wa Messi na Barcelona, alifanya hivyo wiki jana, yapata miezi mitano baada ya kutia mchoro kudumu wa jina Messi kwenye makalio yake. Kulingana naye, maamuzi hayo yalichochewa na imani kwamba Messi ndiye atakayetawazwa mfalme wa Ballon d’Or mwishoni mwa mwaka huu.

“Nina hakika Messi atanyakua taji la Ballon d’Or kwa mara ya sita mwishoni mwa mwaka huu. Michoro hii ya jina lake kwenye ghuba zangu na sehemu nyinginezo za mwili ni kwa minajili ya ‘karamu’ mahsusi ya kumhongera. Naamini mara hii atakuwa mwepesi wa kutikisa buyu hili la asali,” akasema Suzy.

Mbali na mchoro wa jina la Messi na nembo ya FC Barcelona, Suzy aliahidi pia kuchanja chale ya ‘No 10’ kifuani pake ili kuashiria nambari ya jezi inayovaliwa na Messi kambini mwa Barcelona na katika timu ya taifa ya Argentina.

Kipusa huyo mwenye umri wa miaka 29 aligonga vichwa vingi vya habari mnamo 2016 baada ya Antonella Roccuzzo ambaye ni mkewe Messi kumzuia kumfikia mumewe mitandaoni.

Kiini cha hatua hiyo ya Antonella ni mazoea ya Suzy kumtumia Messi picha nyingi za uchi na jumbe za kumtaka kimapenzi.

Katika majaribio mengi ya kumtia Messi kishawishini, Suzy aliwahi pia kuvua nguo na kusalia uchi wa mnyama ili kusherehekea ufanisi wa fowadi huyo katika majukwaa mbalimbali ya soka. Mwishoni mwa mwaka jana, Antonella alimtaka mumewe kukatiza kabisa mawasiliano yote na Suzy au la, aivue pete ya ndoa aliyomvisha rasmi mnamo Juni 2017.

Kulingana na gazeti la The Sun, Antonella anahisi kwamba mumewe huenda akashawishika kutoka kimapenzi na Suzy ambaye hajaficha ? azma ya kumwanikia Messi tunda lake alidokoe.

Mnamo Septemba 2017, Antonella alimshinikiza Messi kutia chale zenye michoro ya midomo yake (Antonella) pajani ili iwe ishara ya kiwango cha ukomavu wa penzi lao!

Pindi alipochora ‘midomo’ ya mkewe katika sehemu za paja lake la kushoto, ilimjuzu Messi kutuma picha kwenye mtandao wake wa Instagram ili kuiridhisha nafsi ya mkewe.

Kilichomkoroga nyongo zaidi Antonella kiasi cha kumuonesha mumewe kadi ya njano, ni hatua ya Messi kumruhusu Suzy kumfikia tena katika mtandao wake wa Instagram baada ya shinikizo la mashabiki kufanikisha kampeni za #UnBlockMeMessi.