Habari MsetoSiasa

Misururu ya kashfa haimbanduki Keter

February 19th, 2018 2 min read

Mbunge wa Nandi Hills, Bw Alfred Kiptoo Keter. Picha/ Maktaba

ALIPOKAMATWA mnamo Ijumaa kwa kuwasilisha stakabadhi zinazodaiwa kuwa ghushi katika Benki Kuu ya Kenya, mbunge Alfred Keter wa Nandi Hills aliongeza msururu wa sakata ambazo zimekuwa zikimwandama.

Bw Keter, alikamatwa na polisi katika majengo ya benki hiyo pamoja na wafanyabiashara wawili; Arthur Ingolo Sakwa na Madat Suburari Chatur kwa madai ya njama ya kuilaghai serikali Sh633 milioni.

Na licha ya hisia kali kutoka kwa baadhi ya wabunge wa Bonde la Ufa kwamba hatua hiyo ni “maonevu” ya wazi dhidi ya mwenzao, hiyo haikuwa mara yake ya kwanza kujikuta katika makabiliano na serikali.

Majuzi, mbunge huyo mbishi alijipata lawamani kwa kukaidi agizo la uongozi wa chama cha Jubilee kujiuzulu kama mwenyekiti wa Kamati ya Bunge kuhusu Masuala ya Leba.

Hii ni licha ya kuraiwa kufanya hivyo na Rais Uhuru Kenyatta na naibu wake William Ruto, ili kutoa usawa katika uongozi wa Jubilee bungeni. Hata hivyo, Bw Keter alikaidi agizo hilo, akidai kwamba Ikulu inaingilia uhuru na utendakazi wa Bunge la Kitaifa.

“Sitajiuzulu. Nilichaguliwa kihalali kama mwenyekiti wa kamati hii. Hatutaruhusu Ikulu ituamulie mpangilio wa uongozi wa bunge, kwani hii ni taasisi huru,” akasema Bw Keter.

Licha ya hayo, aliondolewa katika nafasi hiyo, baada ya wabunge wa kupiga kura ya kutokuwa na Imani naye.

Wabunge wengine waliokaidi agizo hilo ni mbunge wa Moiben, Silas Tiren, David Bowen (Marakwet) na Alex Kosgey wa Emgwen.

 

Ukaidi na vitisho

Mnamo 2015, Keter alinaswa katika video akiwatishia maafisa wa kukagua mizigo katika Kituo cha Kukagua Mizigo cha Gilgil. Aliwatishia kuhusu “hatua kali” ikiwa hawangeruhusu kuachilia lori moja, lililomilikiwa na aliyekuwa mbunge maalum, Bi Sonia Birdi.

Alinukuliwa kwenye video hiyo akisema,”Hizi sheria ni sisi tunaziunda na tunazivunja tutakavyo.”

Mwaka uo huo, Bw Keter alitishia kuwashinikiza wenzake kupiga kura ya kutokuwa na imani, iwapo aliyekuwa Waziri wa Ugatuzi, Bi Anne Waiguru, hangejiuzulu.

Hiyo ni baada ya Bi Waiguru kuhusishwa na sakata ya ufisadi katika Huduma ya Kitaifa kwa Vijana (NYS) ambapo zaidi ya Sh791 milioni zinaaminika kupotea.

Mbali na hayo, aliibuka kama mkosoaji mkuu wa uongozi wa Rais Uhuru Kenyatta pindi Reli ya Kisasa (SGR) ilipoanza kujengwa kwa kudai uwepo wa njama za kuwafilisi Wakenya zaidi ya Sh100 bilioni.

Hata hivyo, serikali illiyataja madai yake kama uongo mtupu. Na licha ya sakata hizo, Bw Keter amekuwa akisisitiza kuwa lengo lake kuu ni “kuwatetea wananchi.”

“Huwa niko tayari kukabiliana na lolote katika kuwatetea wananchi, kwani ndio walinichagua kama kiongozi wao,” akasema Bw Keter.

Mbunge huyo anahudumu katika kipindi chake cha pili, baada ya kuchaguliwa kwa mara ya kwanza mnamo 2013.