Miswada yataka walioshtakiwa wasiwanie viti

Miswada yataka walioshtakiwa wasiwanie viti

Na CHARLES WASONGA

WANASIASA na maafisa wa serikali ambao wameshtakiwa kwa ufisadi sasa watazuiwa kushiriki katika uchaguzi mkuu ujao, ikiwa wabunge watapitisha miswada miwili kuhusu maadili na uteuzi wa wagombeaji.

Mbunge wa Ugunja Opiyo Wandayi, jana alisema ameandaa miswada ya marekebisho ya Sheria za Maadili na Uongozi Bora, 2012 na Sheria ya Uchaguzi, 2011 kuzuia viongozi kama hao kushikilia nyadhifa za umma na kuwania viti katika chaguzi.

Ikiwa miswada hii itapitisha Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) haitaidhinisha washukiwa wa ufisadi kuwania nyadhifa za uongozi katika uchaguzi mkuu ujao.

“Lengo la marekebisho ninayopendekeza kwa sheria hizo ni kuzuia kwa muda maafisa wa serikali (waliochaguliwa na walioteuliwa) ambao wameshtakiwa rasmi kwa ufisadi kuondoka afisini. Vile vile, watu wanaokabiliwa na kesi za ufisadi mahakamani wasiteuliwe kuwa wagombeaji wa nyadhifa mbalimbali katika chaguzi,” Bw Wandayi akasema kwenye kikao na wanahabari katika majengo ya bunge.

“Washukiwa wa ufisadi hawafai kuruhusiwa kushikilia au kuwania nyadhifa za uongozi kabla ya wao kuondolewa lawama na mahakama,” akaongeza.

Bw Wandayi, ambayo pia ni mwenyekiti wa Kamati ya Bunge kuhusu Uhasibu wa Pesa za Umma (PAC), alisema tayari Spika wa Bunge la Kitaifa ameidhinisha miswada hiyo miwili na itawasilishwa bungeni hivi karibuni.

Kulingana na Mbunge huyo, kuwazuia wafisadi kuwania au kuteuliwa kwa nyadhifa za uongozi ndio njia mwafaka itakayoisaidia serikali kufaulu katika vita dhidi ya ufisadi na utekelezaji wa mahitaji ya Sura ya Sita ya Katiba kuhusu maadili.

“Sakata nyingi ambazo zimeripotiwa nchini kwa miaka mingi zinahusisha watu wanaoshikilia nyadhifa za uongozi na wajibu wa kulinda mali ya umma. Watu kama hawa wamegeuka maadui wa taifa hili,” Bw Wandayi akaeleza.

Mbunge huyo ambaye ni Mkurugenzi wa Masuala ya Kisiasa katika chama cha ODM, alisema, Sheria ya Maadili na Uongozi Bora, 2012 ni dhaifu kwa kuwa imeruhusu maafisa na wanasiasa kuendelea kushikilia nyadhifa za uongozi hata baada ya kushtakiwa kwa tuhuma za ufisadi.

“Isitoshe, wengine wakati huu wanaendelea kujiandaa kwa uchaguzi mkuu ujao, ilhali wanakabiliwa na kesi za ufisadi au zinazohusiana na ufisadi. Watu kama hawa hawawezi kutwikwa wajibu wa kutekeleza sheria za maadili na kupambana na ufisadi endapo watachaguliwa,” Bw Wandayi akasema.

Alisema marekebisho anayopendekeza yanaafiki mahitaji ya kipengele cha 10 kuhusu Misingi ya Uongozi Bora, kipengele cha 99 (1) (b) kuhusu sifa za mtu anayehitimu kuchaguliwa kuwa mbunge au diwani.

“Kimsingi nataka kuhakikisha kuwa hitaji ya Sura ya Sita kuhusu Maadili na Uongozi Bora linatekelezwa na kuzingatiwa kikamilifu,” akasema Bw Wandayi.

Baadhi ya viongozi wanaokabiliwa na kesi tofauti nchini ni magavana Okoth Obado (Migori), Muthomi Njuki (Tharaka Nithi), Sospeter Ojaamong (Busia), Moses Lenolkulal (Samburu), Ali Korane (Garissa). Wengine ni wabunge Rigathi Gachagua (Mathira), Patrick Musimba (Kibwezi Magharibi), Alfred Keter (Nandi Hills), James Gakuya (Embakasi Kaskazini), Ayub Savula (Lugari).

You can share this post!

CCM yakataa kuingia UDA

Joho atiwa presha atangaze mrithi wake