Mitaa mitatu Mukuru yakosa maji kwa kipindi cha wiki nzima

Mitaa mitatu Mukuru yakosa maji kwa kipindi cha wiki nzima

Na SAMMY KIMATU

WAKAZI katika mitaa mitatu ya mabanda wanahofia maisha yao kutokana na ukosefu wa maji safi kwa muda wa wiki moja sasa.

Maji hayo huwa yanasambazwa na kampuni ya Nairobi Water.

Mitaa iliyoathirika na uhaba wa maji ni pamoja na mtaa wa Kayaba, mtaa wa Hazina na mtaa wa mabanda wa Maasai ambapo yote iko South B, kaunti ndogo ya Starehe.

“Tangu Jumatatu iliyopita, wakazi wanahangaika mitaani wakitafuta maji ya kunywa kutoka kwingineko. Hali hii inawasukuma wazazi kulazimika kunywa maji kutoka kwa visima vilivyochimbwa mitaani na Idara ya Kutoa Huduma katika Jiji la Nairobi (NMS),” mwenyekiti wa mtaa wa Mukuru-Hazina Bw David Kiarie akanena.

Licha ya maji ya kisima kupatikana kwa wingi katika mtaa wa Kayaba na Hazina, wakazi wanasema kuwa maji hayo ni ya chumvi.

“Watu huku hawachemshi maji haya ya chumvi wala kuyatia dawa kabla ya kunywa. Tunahofia mkurupuko wa maradhi yanayotokana na maji kufuatia kuadimika kwa maji safi mitaani,” Bi Jane Mbula, mhudumu wa afya mtaani Kayaba akanena.

Hata hivyo, baadhi ya wakazi waliozungumza na Taifa Jumapili walisema maji ya kisima kwa kawaida huwa wanayatumia kufulia nguo na kupiga deki nyumbani wala sio ya kunywa.

  • Tags

You can share this post!

Bayern na Lewandowski waweka rekodi mpya za ufungaji wa...

Wakulima warai Munya aingilie kati kuhusu deni

T L