MITAMBO: Bailers za kisasa zinazotumia GPS

MITAMBO: Bailers za kisasa zinazotumia GPS

NA RICHARD MAOSI

KULISHA mifugo kunahitaji mambo mengi kuzingatiwa.

Mfugaji anapaswa kufahamu kuwa ni jambo la kimsingi kwa wanyama kupata lishe yenye virutubisho muhimu vya protini, vitamini na wanga.

Lishe bora zitawasaidia mifugo kukua haraka na kudhibiti maradhi kwa kuimarisha kinga mwilini, hii ni kwa sababu elimu ya kutosha inabakia kuwa mhimili mkubwa wa kufanikisha haya maana ubora wa chakula cha mifugo unategemea mbinu ya uzalishaji.

Mfugaji atalazimika kuchunguza kwa kina elimu za teknolojia ya kisasa kwa mfano kuvumbuliwa kwa kifaa cha GPS Bailers, kinachotoa mwongozo wa fomula maalum za kuchanganya aina mbalimbali za lishe.

Bailers za kisasa

Mtaalamu wa trekta Vincent Sifunya kutoka ICS Agric Kenya anasema kuwa trekta inaweza kukokota mtambo wa bailer ambao aghalabu hutumika kufunga na kutengeneza lishe ya hay.

Alifichulia Akilimali kuwa mtambo wenyewe umeboreshwa na kufanyiwa marekebisho kwa kutumia ubunifu.

Pamoja na gharama kubwa inayowakumba wakulima kwa kuajiri vibarua wakati wa kuvuna nyasi, matumizi ya bailers za kisasa ni ya haraka na nafuu na vilevile husaidia kupunguza uharibifu wa mazao.

Sifunya anasema bailer ya kisasa tofauti na ile ya jadi inaweza kuvuna, kupakia na kutengeneza maumbo mstatili ya hay, katika kipindi cha muda mfupi sana.

Vincent Sifunya akiwa miongoni mwa wakulima wengine wakati wa kuvuna ngano kwa kutumia bailer ya kisasa inayotumia GPS na hatimaye kubururwa na trekta. PICHA | RICHARD MAOSI

Mbali na kutengeneza lishe za hay, uvumbuzi mpya katika matumizi ya aina mpya ya mtambo wa bailer unaonyesha kuwa ni mtambo ambao unaweza kuchanganya aina mbalimbali ya majani kwa fomula maalum.

Sifunya anasema siku za hivi karibuni hay na silage zimetokea kuwa mojawapo wa lishe maarufu kwa wakulima wadogo na wale wenye mashamba makubwa.

Wafanyabiashara pia wamejitokeza kwa wingi kujihusisha na kilimo biashara hiki wakilenga masoko ya mbali na karibu, wengi wao wakitumia mtambo wa bailer.

Ingawa walikuwa wakitegemea bailers za zamani ambazo hazikuwa na programu ya kutoa maelezo ya kina kuhusu shamba, mazao wala eneo la ukulima.

Francis Malemba Kyondo, afisa wa KALRO akionyesha mtambo wa Bailer ya zamani. PICHA | RICHARD MAOSI

Ikumbukwe kuwa mtambo wa kisasa wa bailer umeboreshwa ikiwa ni baada ya kuwekewa kifaa cha programu ya ramani ya kimaeneo almaarufu kama GPS, ili kufanya kilimo kiwe chenye tija.

Anasema kuwa GPS katika kilimo cha kisasa husaidia kutoa kumbukumbu na kuonyesha ramani ya sehemu mbalimbali katika shamba.

“Aidha bailer ya kisasa hutoa maelezo kuhusu udongo, kiwango cha mazao, ikiwa ni pamoja na habari za kijiografia,” asema.

Hivyo basi, mtambo wa kisasa wa bailer unaotumia GPS unaweza kumsaidia mkulima kufanya mahesabu yake ili aelewe endapo anatengeneza faida ama hasara.

Isitoshe, matofali haya ya lishe yanaweza kuchanganywa na aina nyingine ya lishe zenye virutubisho kama vile lucerne, viazi vitamu na silage.

Sifunya anaungama ni kifaa ambacho kinawasaidia wakulima kuimarisha malezi ya mashamba kwa wakulima wadogo, ikizingatiwa kuwa husaidia kutunza mazingira kwa kutoa taarifa kuhusu shamba.

  • Tags

You can share this post!

ZARAA: Teknolojia ndio itaokoa kilimo nchini, afisa asema

UJASIRIAMALI: Uraibu wa kuoka wageuka biashara

T L