MITAMBO: Commercial milk coolers husaidia kuhifadhi maziwa na kupunguza hasara

MITAMBO: Commercial milk coolers husaidia kuhifadhi maziwa na kupunguza hasara

NA RICHARD MAOSI

ENEO la Afrika Mashariki na Kati lina soko la maziwa lililoshamiri kutokana na upatikanaji wa teknolojia bora na endelevu katika vituo vya kupokea maziwa kabla ya kuyasafirisha viwandani.

Karibu kila boma katika maeneo ya mashambani humiliki ng’ombe, kuna bidhaa nyingi ambazo zinaweza kutengenezwa kutokana na maziwa kama vile samli, siagi na maziwa mala.

Msimu wa kiangazi bei ya maziwa ghafi hupanda na kufikia hadi Sh60 kwa lita, ndiposa wafugaji hujaribu kila mbinu kuhakikisha upatikanaji wa bidhaa hii adimu, ili kukidhi mahitaji ya watumiaji.

Hata hivyo, bidhaa hii huwa ya kuharibika haraka na wakulima kutoka maeneo ya Uasin Gishu, Nyandarua, Kiambu, Baringo, Kericho na Bomet wanashauriwa kutumia mtambo wa milk coolers ili kuhifadhi maziwa yao kwa muda mrefu yasije yakaharibika wanapokosa soko.

“Ni mtambo unaotumika kuhifadhi lita nyingi za maziwa hususan miongoni mwa wakulima ambao wanaendesha ufugaji katika makundi ya ushirika,” anasema Joshua Tenai mtaalam wa Teknoloji ya Kilimo cha Ufugaji kutoka Kaunti ya Nandi.

Kupitia mtambo wa milk coolers, visa vya matapeli kuchuuza maziwa duni mitaani vitapungua ikiwa ni pamoja na kupiga marufuku tabia ya kuongeza unga, sukari maji au mayai ndani ya maziwa ghafi.

“Mradi mkulima azingatie utaratibu wa kusafisha vyombo vya kukusanya na kuhifadhi maziwa kuanzia vipimo vya kimsingi ambavyo ni kuangalia na kunusa,” anaeleza.

Anasema kuwa kabla ya wakulima wengi kukumbatia mfumo huu wa kuhifadhi maziwa, walikuwa wakitumia njia za rejareja kuyauza maziwa yao jambo ambalo hufanya kiwango cha usafi kuzorota, ikizingatiwa kuwa wengi wao hutumia vyombo vya plastiki wakati wa kukama.

“Wanunuzi wamekuwa wakimwaga maziwa yao pindi tu yanapoharibika jambo ambalo huwafanya wauzaji kukadiria hasara kubwa,” anasema.

Lakini kupitia mtambo wa commercial milk coolers machine, mkulima anaweza kuyahifadhi maziwa yake baina ya muda wa saa 48-72 kabla ya kufikishwa sokoni.

Kulingana na Tenai ni teknolojia ambayo imekuwa ikiwasadia wakulima kupata muda wa kutosha kutafuta soko kwa bidhaa zao, na hivyo mkulima anaweza akayauza maziwa yake kwa hela nzuri.

Akilimali vilevile ilipata fursa ya kutembelea mkulima Francis Mwangi kutoka eneo la Muwa Lanet ambaye alitufichulia namna ambavyo amekuwa akifaidi kutokana na matumizi ya mtambo wa milk coolers.

Mwangi anasema yeye hukama mara tatu kwa siku, kila baada ya muda wa saa nane na kwa siku moja anaweza kupata kati ya lita 750-770 za maziwa kutoka kwa ng’ombe 31 anaokama kati ya mifugo 110 alio nao, ambapo lita moja huuzwa Sh54.

Mfanyakazi akitumia commercial milk coolers, mitambo ambayo huhifadhi zaidi ya lita 4,000 za maziwa yakisubiri kufikishwa hadi sokoni. PICHA | RICHARD MAOSI

Kwa sababu wanunuzi wake wengi ni kutoka kaunti jirani ya Nairobi, aliona haja ya kuwekeza katika teknolojia ya kuhifadhi maziwa ambapo anamiliki mitambo miwili , ikiwa kwa ujumla anaweza kuhifadhi zaidi ya lita 4, 100 .

Kulingana na Mwangi, maziwa yanaweza kudumu ndani ya coolers kwa siku mbili kabla ya kuchukuliwa na wanunuzi kutoka Nairobi, na kila siku amelazimika kuhifadhi kumbukumbu ya rekodi za ukamaji ng’ombe.

Alieleza kuwa kifaa hiki hudumisha usafi na mtambo wenyewe umekuwa ukimsaidia kuepuka hasara hasa wakati ambapo maziwa yanakuwa mengi.

Pia anasema kuwa mtambo huo umempa motisha ya kuongeza uzalishaji ili kutosheleza mahitaji ya soko na kwa wakati huo kutoa ajira kwa vijana ambao baadhi wamehitimu kutoka vyuoni.

  • Tags

You can share this post!

UJASIRIAMALI: Alikuwa mchuuzi tu, sasa aagiza mitumba...

IEBC yakosa kutaja vituo visivyo na mfumo wa kisasa kutuma...

T L