Akili Mali

Mitambo: ‘Kisiagi’ cha uchumi wa ‘kadogoo’ kisichopiga kelele

April 26th, 2024 2 min read

NA LABAAN SHABAAN

WAKATI huu ambapo gharama ya maisha inapanda na mja anahitaji kutumia muda mwingi kujitafutia riziki, anahitaji mtambo wa kurahisisha shughuli.

Wapenda ugali wasiopenda kupanga foleni wakienda kwa kisiagi cha mahindi kupata unga, sasa wanaweza kununua mtambo huo mdogo kujisagia unga wakiwa nyumbani kwao.

Aidha, badala ya mtambo wa kusaga nafaka na mazao mengine ya shambani unaotumia dizeli pekee au stima pekee, kisiagi cha kadogoo kinampa mtumiaji chaguo la kutumia nishati kutokana na miale ya jua na stima.

Mvumbuzi Diana Moshono atia nafaka kwenye faneli ya mtambo wa kisiagi cha kutumia sola. PICHA | LABAAN SHABAAN

Kisiagi kinachotumia dizeli kimekuwa na matokeo mabaya wakati mwingine ikitokea kwamba anayesimamia shughuli atakosa kudumisha usafi ambapo kinaweza kusaga unga wa sima na kuacha harufu ya mafuta.

Bi Diana Moshono ambaye ni mvumbuzi mbunifu anapigia debe matumizi ya kawi safi na jamii kukumbatia mitambo hii midogo yenye kutumia nguvu za jua na umeme.

“‘Kisiagi cha kadogoo’ ni bora kwa sababu hutumia nafasi ndogo na nishati, hakipigi kelele wala kutetemesha sakafu na pia kinaweza kujiwasha na kujizima,” anaeleza Bi Moshono.

“Mtambo huu unaweza kufaa matumizi ya nyumbani, shambani na pia biashara ya kusaga chakula,” anaongeza.

Kwa mujibu wa Bi Moshono, mtambo huu mdogo unaweza kuwafaa wakulima wa kiwango cha kadri wanaokuza mimea na kufuga ng’ombe, mbuzi na kondoo.

Ni mashine yenye uwezo wa kusaga mahindi na mazao mengine kwa ajili ya malisho ya mifugo kwa kubadili miundo.

Bi Diana Moshono aonyesha vichungi vinavyotumiwa kuchuja mazao wakati wa uchakataji. PICHA | LABAAN SHABAAN

Wakati uo huo, mtambo huu hutumiwa kusaga nafaka kwa ajili ya mapishi nyumbani.

“Ukijinunulia mtambo huu nyumbani, unaweza hata kufanyia biashara sababu unabebeka,” anaeleza Bi Moshono akimtaja mmoja wa wateja wake ambaye huubeba kutoka sehemu moja hadi nyingine.

Kisha anaongeza: “Uzuri wa maendeleo ya teknolojia ni kwamba una chaguo la kutumia miale ya jua – ambayo haina gharama – ama utumie umeme kuendesha mtambo huu.”

Bi Moshono anafafanua kuwa kifaa hiki huchakata nafaka kupatikana unga wa kilo 50 kwa saa moja na malisho ya mifugo kilo 250 kwa muda uo huo.

Kifaa hiki kinagharimu angalau Sh70,000 na wito unatolewa kwa familia kuukumbatia kwa wingi kuboresha maisha nyumbani na shambani.