Makala

Mitandao ya kijamii hatarini kufungwa Uingereza

January 29th, 2019 2 min read

MASHIRIKA Na PETER MBURU

SERIKALI ya Uingereza imetishia kupiga marufuku kampuni za mitandao ya kijamii, ikiwa hazitatoa jumbe ambazo zinawezakuwa hatari kiafya.

Waziri wa Afya Andrew Marr ameeleza kuwa kampuni hizo zikikosa kufuata maagizo ya serikali, sheria itapitishwa kuzipiga marufuku.

“Ikiwa tutaona kuna kitu wanafaa kufanya ambacho wanakataa, tutafunga na sharti tutunge sheria,” akasema Marr.

Lakini alishauri kampuni hizo kushirikiana na serikali, kwa lengo la kuzuia jumbe ambazo zinawezakusababisha watu kujiumiza ama kujiondoa uhai, baada ya tineja mmoja kujiua.

Alipoulizwa ikiwa kuna uwezekano wa mitandao ya kijamii kupigwa marufuku, Bw Hancock alisema “bunge lina huo uwezo, ndio” japo akaongeza kuwa “lakini hatungependa kuishia hapo.”

Msichana Molly Russel wa miaka 14 alijitoa uhai mnamo 2017 baada ya kutazama ujumbe uliomsumbua kuhusu kujiua.

Babake mtoto huyo alieleza kuwa anaamini mtandao wa Instagram “ulichangia kumuua mwanangu.”

Bw Russel, babake tineja huyo aidha alikashifu chapisho la Pinterest kuwa pia lilichangia.

Lakini mtandao wa Instagram ulisema kuwa huwa hautoi jumbe fulani ambazi zinaweza kuwafaa watu wengine wanapoziona.

Instagram aidha ilisema kuwa inakagua sera zake za utendakazi na teknolojia.

Mtandao wa Facebook nao uliomba msamaha kwa hilo, kwani ndio unamiliki Instagram. Wasimamizi wake walisema kuwa jumbe zinazoweza kusababisha mtu kujiumiza “hazina nafasi katika mtandao wetu.”

Wazazi nchini humo wameeleza kuwa vijana wanafaa kulindwa kwani wamekuwa wakiadhiriwa na jumbe za mitandao.

“Tumekuwa tukipokea simu kutoka kwa watu wanaolalamika kuhusu mambo hayo,” akasema msemaji wa shirika moja la kusaidia jamii.

Waziri naye alitumia mitandao ya Twitter, Snapchat, Pinterest, Apple, Google na Facebook barua, akipongeza hatua ambazo tayari zimechukua, na kutaka zizidi kuchukua nyingine zaidi.

“Inashangaza jinsi bado watu wanaweza kukumbana na jumbe hizi mitandaoni na sina shaka kuwa zinaweza kuadhiri mtu vibaya, haswa vijana,” waziri huyo akasema.

“Wakati umefika kwa intaneti na wahudumu wa mitandao ya kijamii kuondoa jumbe hizi kabisa,” akaendelea.

Aliongeza kuwa serikali inaunda nakala ya kutoa mwelekeo kuhusu athari zinazopatikana mitandaoni, akisema masuala ya kujiua na kujijeruhi yataangaziwa.

Serikali ilisema japo wazazi wengi wameshindwa kukabili changamoto zinazowakumba wanao, haitashindwa kufanya hivyo.