Makala

MITCHELL WAMBUI: Waliobobea kwa filamu wainue waigizaji chipukizi

November 11th, 2020 2 min read

Na JOHN KIMWERE

UKWELI wa mambo ni kwamba wahenga waliposema penye nia pana njia hawakupaka mafuta kwenye mgongo wa chupa, maana ndivyo ilivyo tangu zama hizo mpaka sasa.

Usemi huo umeonyesha mashiko ya haja miongoni mwa jamii. Aidha ni msemo unaozidi kudhihirishwa na wengi ambao wameamua kujituma kisabuni kwa kujiamini wanaweza huku wakilenga kutimiza malengo yao maishani.

Miongoni mwao ni Mitchell Wambui Kamau ambaye ni mwigizaji anayeibukia. Ingawa ndio ameanza kupiga ngoma kisura huyu aliyetua duniani mwaka 1998 ni msomi wa mwaka wa tatu anakolenga kuhitimu kwa shahada ya digrii kama mwana habari wa televisheni.

Hata anasema tangia akiwa mtoto amekuwa na ndoto ya kuhitimu kuwa wakili kama taaluma yake lakini hali imekwenda mrama. Kipusa huyu ambaye kisanaa anafahamika kama Kenzi anasema ”Ingawa sijapata mashiko katika masuala ya uigizaji ninaamini nina talanta ya kufanya vizuri katika jukwaa hili.”

Ni takribani mwaka mmoja tangia kipusa huyu aanze kujituma katika masuala ya filamu. Hata hivyo anasema ndani ya miaka mitano ijayo imepania kufikia upeo wa waigizaji wa kimataifa na kutinga kiwango cha Hollywood.

Kipusa huyu anayejivunia kushiriki filamu moja kwa jina ‘Mpango wa kando’ anasema kila jambo huanza kwa hatua moja anakoamini ipo siku atafanikiwa kutikisa jukwaa la wana maigizo. Anadokeza kuwa alipata motisha kuanza kukuza kipaji chake alipotazama filamu iitwayo ‘Kina’ aliyoigiza msanii Sanaipei Tande. “Hadi sasa binfasi napenda kutazama filamu za mwana dada huyo,” akasema.

PEARL NTHUSI

Katika mpango mzima kisura huyu anadokeza kuwa anapania kumiliki brandi yake miaka ijayo ili kusaidia waigizaji wa kike wanaokuja. Anasema kwamba waigizaji wa kike ambao hawajapiga hatua kubwa katika maigizo kwao huwa vigumu kupata ajira ya uigizaji. Anakariri kwamba kamwe maprodusa hawastahili kudharau wanamaigizo wanaokuja maana ndio watakaotwaa nafasi za wenzao wakiondoka duniani.

Kwa wenzake waliokomaa Afrika anasema angependa kufanya kazi na mwigizaji mahiri Pearl Nthusi mzawa wa Afrika. Nthusi ni kati ya waigizaji mahiri nchini humo anakojivunia kushiriki filamu kama ‘Queen Sono,’ ‘Catching feelings,’ na ‘Quantico’ kati ya zingine. Kwa waigizaji wa nyumbani binti huyu anasema anatamani kujikuta jukwaa moja na wenzake kama Makena Kahuha na Kate Actress kati ya wengine.

CHANGAMOTO

Anasema kwa waigizaji wanaokuja huwa vigumu kupata nafasi ya ajira maana maprodusa wengine hupenda kuwapa nafasi wenzao waliowatangulia.

”Binafsi ningependa kutoa mwito kwa wenzetu waliokomaa katika sekta ya uigizaji watushike mkono ili tupaishe jukwaa la maigizo nchini na kutoa ajira kwa chipukizi waliofurika katika kila kona ya taifa hili,” akasema.

Ili kuepuka mitego ya wanaume ambao hupenda kuwashusha wanawake chipukizi huyu ashauri wenzie wajifunze kujiheshimu pia kufahamu wanachotaka katika sekta ya uigizaji.