Habari Mseto

Mitihani ya mwigo yapigwa marufuku Baringo

June 5th, 2018 1 min read

Na Florah Koech

SERIKALI imepiga marufuku mitihani ya pamoja ya majaribio almaarufu ‘Mock’ katika shule za upili za Kaunti ya Baringo.

Akihutubia mkutano wa chama cha walimu wakuu wa shule za sekondari (KESHHA) mjini Kabarnet, Mkurugenzi wa Elimu wa kaunti hiyo Bw Willie Machocho alihusisha mitihani hiyo na visa vya migomo shuleni.

Alisema wanafunzi wengi katika eneo hilo hugoma wakati wa maandalizi ya mitihani hiyo.

“Shule kadhaa eneo hili zimekumbwa na ghasia kwa sababu ya maandalizi ya mitihani hii. Kwa sababu hii, tunapiga marufuku mitihani yote ya majaribio katika shule zote za sekondari ili kuzuia hali hiyo,” alisema Bw Machocho.

Alitaja shule zilizogoma muhula huu kama ya wavulana ya Tenges, Reuben Cheruiyot, Maji Moto , Rosoga, Kisanana na Timboroa.

Alisema mbinu nyingine ambayo wanatumia kuzima migomo ya kila mara ni kuhakikisha walimu wakuu na manaibu wao wanaishi shuleni

Tangazo hilo lilijiri wiki mbili baada ya mali ya mamilioni ya pesa kuteketea katika bweni la shule ya wavulana ya Tenges iliyoko Baringo ya Kati. Moto huo ulizuka wanafunzi walipokuwa madarasani jioni.

Visa vingi vya migomo hushuhudiwa muhula wa pili kutokana na kile washikadau katika elimu wanahusisha na mitihani ya mwigo.