Habari

Mitihani yaja walimu, wanafunzi wakiteseka

October 18th, 2019 2 min read

Na WAANDISHI WETU

HATIMA ya maelfu ya walimu na wanafunzi haijulikani huku serikali ikiendelea na operesheni ya kufunga shule ambazo hazijatimiza masharti na kanuni za usalama kote nchini.

Walimu ambao kufikia sasa wameachwa bila ajira hawana uhakika ikiwa shule hizo zitafunguliwa na endapo watahifadhi kazi zao.

Maelfu ya watahiniwa wa mitihani ya kitaifa ya darasa la nane (KCPE) na ile ya kidato cha nne (KCSE) ambao shule zao zimefungwa wameathirika pakubwa kwa kukosa mazingira faafu ya kujiandaa vizuri kwa mitihani hiyo.

Septemba, Wizara ya Elimu iliamuru maafisa wake kukagua majengo ya shule zote nchini kubaini ikiwa yalijengwa kwa kufuata kanuni za ujenzi.

Pia maafisa hao wamekuwa wakichunguza ikiwa shule zote humu nchini zimesajiliwa na wizara inavyohitajika. Isitoshe, maafisa hao wanapaswa kuhakikisha kuwa walimu wanaofundisha katika shule zote za umma na binafsi wamesajiliwa na Tume ya Huduma kwa Walimu (TSC).

Amri yatolewa na waziri

Amri hiyo ilitolewa na Waziri wa Elimu Prof George Magoha kufuatia kisa cha kuporomoka kwa darasa katika Shule ya Msingi ya Precious Talent Academy, Nairobi ambapo wanafunzi wanane walifariki na wengine 54 kujeruhiwa.

Baada ya kuamuru kufungwa kwa shule zisizoafikia kanuni za usalama, maafisa hao huagiza kwamba wanafunzi wahamishiwe shule jirani.

Operesheni hiyo inatarajiwa kufikia kikomo Ijumaa wiki ijayo shule zitakapofungwa. Kisha ripoti itatayarishwa na kuwasilishwa kwa Katibu wa Wizara ya Elimu Belio Kipsang kufikia Oktoba 31, 2019.

Watahiniwa wa KCPE na KCPE pia wamehamishwa hadi shule nyingine na hawatakuwa na muda wa kutosha kuzoea mazingira mapya, kwani mitihani hiyo inatarajiwa kuanza baada ya wiki moja.

Uhamisho huo wa wanafunzi umezidisha changamoto za msongamano na uhaba wa walimu katika shule zilizopokea wanafunzi wageni.

Kuzorota kwa hali katika shule zilizofungwa kunachangiwa na uzembe wa idara ya kudumisha ubora ambayo imetwikwa wajibu wa kukagua shule kila mara kuhakikisha zinatimiza viwango vinavyohitajika.

Ni mwezi mmoja tangu maafisa wa idara hiyo waende nyanjani kukagua maelfu ya shule.