MakalaSiasa

Mivutano ya UhuRaila, Tangatanga kuwanyima haki watu wa Kirinyaga

June 20th, 2020 3 min read

Na CHARLES WASONGA

MCHAKATO wa kuchunguza madai yaliyotolewa dhidi ya Gavana Anne Waiguru na madiwani wa Kirinyaga wanaotaka abanduke tayari umetekwa na mvutano wa siasa kati ya Rais Uhuru Kenyatta na Naibu Rais William Ruto.

Hali hii inatarajiwa kuvuruga haki katika mchakato huo.

Wadidisi wanasema inasikitisha kuwa madai ya ufisadi dhidi ya Bi Waiguru sasa yamegubikwa na siasa za ubabe kati ya mirengo ya ‘handisheki’ na ‘tangatanga’ ilivyodhihiri katika Seneti mnamo Jumanne wakati wa kubuniwa kwa kamati ya kusikiza madai dhidi ya Bi Waiguru.

Maseneta waligawanyika kwa misingi ya mirengo hiyo miwili, ambapo Jubilee na Nasa walitetea kuundwa kwa kamati maalum ya kuchunguza madai dhidi ya Waiguru na ukaibuka mshindi kwa kura 45.

Nao upande uliotaka suala hilo lishughulikiwe katika kikao kizima cha Seneti ulijumuisha wandani wa Naibu Rais William Ruto, ambao walilemewa baada ya kupata kura 14 pekee.

Taswira iliyojitokeza ni kwamba Gavana Waiguru alipata ushindi wa kwanza kutokana na kuwa ni rahisi kwa wanachama 11 wa kamati hiyo “kushawishiwa” kwa urahisi kumtakasa Bi Waiguru.

Kimsingi, suala hilo sasa limechukua mwelekeo wa siasa za kitaifa, wala sio masuala yanayowahusu wakazi wa Kirinyaga, haliambayo itayeyusha masuala muhimu katika hoja hiyo.

Wakili na mchanganuzi wa masuala ya kisiasa George Ogola, anaonya kuwa uwepo wa mivutano kuhusu suala hilo lenye uzito kwa wakazi wa Kirinyaga itawanyima haki.

“Inasikitisha kuwa tayari kuna madai kuwa makundi haya mawili yalifanya mikutano ya kujadili namna ya kufanikisha malengo yao. Mrengo wa handisheki ulisemekana kukutana kupanga namna ya kumnusuru Waiguru huku wapinzani wao wakipanga namna ya kumsulubisha,” anasema.

Siku chache kabla ya hoja hiyo kusomwa rasmi katika Seneti, Bw Odinga, na wandani wake, waliripotiwa kukutana na Gavana Waiguru katika mkahawa mmoja mtaani Karen kupanga mikakati ya kumwondolea lawama.

Ingawa Bw Odinga alikana ripoti hizo, mwandani wake wa karibu, Junet Mohammed, alitangaza hadharani kuwa chama cha ODM kimeamua “kusimama” na Bi Waiguru bila kujali madai dhidi yake.

Siku moja baada ya mkutano huo, Dkt Ruto naye aliongoza mkutano wa maseneta 16 katika makazi yake rasmi katika mtaa wa Karen, ambapo ajenda kuu ilikuwa na suala lilo hilo la hoja ya kumtimua Bi Waiguru afisini.

Duru kutoka mkutano huo zilisema kuwa Naibu Rais aliwataka maseneta hao, wakiongozwa na seneta wa Elgeyo Marakwet Kipchumba Murkomen, kuhakikisha kuwa “Waiguru anaangushwa au kuokolewa kwa misingi ya namna atakavyojitetea dhidi ya makosa aliyodaiwa kutenda.”

Wanaodaiwa “kudhamini” msukumo wa kutimuliwa kwa Waiguru mashinani katika kaunti ya Kirinyaga ni pamoja na Naibu wake Peter Ndambiri, Mbunge Mwakilishi wa Wanwake Wangui Ngirici, kiongozi wa Narc Kenya Martha Karua na Katibu wa Wizara ya Usalama Karanja Kibicho.

Hata hivyo, Dkt Kibicho amekana madai hayo akisema yeye ni mtumishi wa umma na haruhusiwi kushiriki mieleka ya kisiasa.

HANDISHEKI KIZINGITI KWA UTAWALA BORA

Mchanganuzi wa masuala ya kisiasa, Javas Bigambo anakubaliana na kauli ya Wakili Ogola kwamba misimamo kinzani ya kisiasa ndiyo inatilia shaka uwezekano wa seneti kuishughulikia suala hilo kwa njia huru.

“Madai ya Seneta Orengo kwamba wale wanaotafuta kichwa cha Waiguru hawako katika bunge la kaunti ya Kirinyaga bali wako kwingineko, yalikuwa mazito mno,” anasema Bw Bigambo.

Madai ya Seneta huyo wa Siaya yamewatia hofu madiwani wa Kirinyaga, viongozi wa eneo hilo na mrengo wa Tangatanga ndani na nje ya seneti, kwamba mrengo Rais Kenyatta, Odinga na Kalonzo Musyoka utatumia ushawishi wake kumnusuru Gavana Waiguru.

Hii ndio maana madiwani 23 wakiongozwa na kiongozi wa wengi Kamau Murango walisema hata kama Seneti itamwokoa Bi Waiguru watapambana naye mashinani.

“Tunaweza kuwasilisha hata hoja kumi za kumwondoa mamlakani; hatutachoka,” akasema.

Naye diwani wa wadi ya Mutira David Kinyua Wangui, aliyedhimini hoja hiyo akaongeza: “Ni wazi kwamba kuna njama ya kutupilia mbali uamuzi wetu kama bunge la Kirinyaga. Uhuru na Raila wanafaa kuelewa kuwa hata kama wakimwokoa Waiguru katika Seneti atarudi nyumbani na tutamfunza adabu”.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Narc-Kenya Bi Martha Karua, anataja mipango ya kumnusuru Gavana Waiguru kama ithibati kuwa muafaka kati ya Rais Kenyatta na Bw Odinga hauna nia ya kusaidfia katika vita dhidi ya ufisadi na maovu mengine ya kiutawala.

“Sasa ni wazi kuwa wao ndio kizingiti kikuu katika vita dhidi ya ufisadi,” anaongeza.

Huku wingu la siasa likigubika mchakato wa kusaka ukweli kuhusu madai dhidi ya Bi Waiguru kupitia Seneti, Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) imeanza kumchunguza gavana huyo na bunge la kaunti ya Kirinyaga kuhusiana na sakata ya upeanaji zabuni na ulipaji marupurupu kinyume cha sheria.

Meneja wa tume hiyo katika eneo la Kati, Charles Rasugu wiki jana aliwaambia wanahabari kuwa malalamishi dhidi ya Bi Waiguru yanahusiana na utoaji wa zabuni ya thamani ya Sh50 milioni na kupokea malipo ya Sh10.6 milioni ya safari hewa ya kigeni.

Watu wa Kirinyaga sasa watasubiri matokeo ya uchunguzi huu wa EACC kupata ukweli kuhusu sakata hiyo kwani mchakato wa Seneti tayari umezamishwa ndani ya bahari ya siasa.