Mivutano yatishia kampeni za Ruto

Mivutano yatishia kampeni za Ruto

NA WANDISHI WETU

KAMPENI za Naibu Rais William Ruto zimo kwenye hatari ya kusambaratika katika baadhi ya maeneo kutokana na mivutano ndani ya washirika katika muungano wa Kenya Kwanza.

Hali imezorota hivi kwamba baadhi ya wanasiasa waliotwikwa jukumu la kuongoza kampeni za Kenya Kwanza kimaeneo sasa wameanza kupigia debe wawaniaji wa muungano pinzani wa Azimio la Umoja One Kenya.

Kati ya wale ambao walitegemewa kuongoza kampeni za Dkt Ruto lakini sasa wanafanyia kampeni wawaniaji wa vyama pinzani ni Gavana Moses Lenolkulal wa Samburu, aliyekuwa gavana wa Kiambu William Kabogo, Mbunge wa Bahati Kimani Ngunjiri na mwaniaji wa useneta wa Kakamega Boni Khalwale.

Mnamo Jumapili, Bw Kabogo alimkana hadharani Dkt Ruto wakati wa mdahalo wa wawaniaji wa ugavana wa Kiambu akisema kuwa amejiondoa kwenye muungano wa Kenya Kwanza.

Uhasama baina ya Bw Kabogo na Dkt Ruto uliibuka wiki tatu zilizopita baada ya kiongozi huyo wa chama cha Tujibebe Wakenya, kulalamika kuwa walipendelea mpinzani wake Kimani Wamatangi wa chama cha United Democratic Alliance (UDA).

Bw Kabogo pia alidai kuwa uteuzi wa Mbunge wa Mathira Rigathi Gachagua kuwa mwaniaji mwenza wa Dkt Ruto umesababisha umaarufu wa Kenya Kwanza kudidimia katika eneo la Mlima Kenya.

Dkt Ruto alikuwa amemweka Bw Kabogo kwenye kikosi cha kampeni kinachoongozwa na kinara wa ANC Musalia Mudavadi. Viongozi wengine katika kikosi hicho ni magavana Okoth Obado (Migori), Samwel Tunai (Narok), maseneta Kithure Kindiki (Tharaka Nithi), Kipchumba Murkomen (Elgeyo Marakwet) na wabunge Ndindi Nyoro (Kiharu) na Catherine Waruguru (Laikipia).

Kwa upande wake, Bw Lenolkulal, ambaye Dkt Ruto alimteua kujiunga na kikosi chake cha kampeni, amekuwa akipigia debe wawaniaji wa ugavana na useneta wa Azimio, Dkt Richard Lesiyampe na Henry Lengolos mtawalia dhidi ya wale wa chama cha UDA, Jonathan Lati Leleliit na Steve Lelegwe mtawalia.

UHASAMA

Taifa Leo imebaini kuwa Bw Lenolkulal amehepa wawaniaji wa UDA kutokana na uhasama wa muda mrefu baina yake na Seneta Lelegwe.

Hii inatia kampeni za Dkt Ruto katika hali ya mshikemshike ikizingatiwa kuwa Samburu ni miongoni mwa kaunti zilizo na ushindani mkali baina ya Dkt Ruto na mwaniaji wa urais wa Azimio Raila Odinga.

Katika Kaunti ya Nakuru, Bw Kimani wa UDA amekuwa akitapatapa, ambapo awali alimuidhinisha Gavana Lee Kinyanjui anayetetea kiti chake kupitia Jubilee dhidi ya mwaniaji wa tiketi ya UDA, Susan Kihika. Baadaye aliahidi kuunga mkono Bi Kihika.

Katika Kaunti ya Kakamega, Bw Khalwale sasa anapigia debe mwaniaji wa ugavana wa ODM, Fernandes Barasa dhidi ya mwenzake wa Kenya Kwanza, Cleopas Malala.

Wawili hao sasa wanaandaa mikutano tofauti tangu wafuasi wa Bw Malala kumtimua Bw Khalwale kutoka kwenye mkutano mapema mwezi huo kwa kuwataka wakazi kuchagua yeyote kati ya seneta huyo na Bw Barasa.

Kiongozi wa The Service Party (TSP) Mwangi Kiunjuri, ambaye ni mmoja wa vinara wa muungano wa Kenya Kwanza pia ameonekana kutapatapa.

Bw Kiunjuri wiki iliyopita alinukuliwa akiambia wakazi wa Laikipia kuchagua mwaniaji wa urais wanayetaka huku akimshutumu Bw Gachagua kwa madai ya kunyanyasa vyama tanzu vya Kenya Kwanza.

Anasema kuwa Bw Gachagua amekuwa akiwanyima vinara wengine wa muungano huo fursa ya kuzungumza katika mikutano ya kisiasa.

“Baadhi yetu ndani ya huu muungano tumehangaishwa na kukasirishwa kiasi kwamba tunakaribia kufika mwisho. Huo ndio utakuwa mwisho wa Kenya Kwanza,” alisema Bw Kiunjuri alipokuwa akihojiwa na kituo cha redio cha Inooro hivi majuzi.

Leonard Onyango, Geofrey Ondieki na Eric Matara

  • Tags

You can share this post!

KINYANG’ANYIRO 2022: Kaunti ya Kisumu

Mwigizaji Michelle Wanjiku apania kufuata nyayo zake Lupita...

T L