Makala

Mizabibu inamhakikishia mkulima faida tele

March 20th, 2019 3 min read

Na SAMMY WAWERU

ZABIBU ni matunda madogo yenye umbo la mviringo na hupatikana kwa rangi mbalimbali hasa kijani, manjano, zambarau, nyeusi, na nyekundu vilevile.

Mbali na kuliwa, zinatumika kutengeneza jemu, sharubati, jeli, dawa, mvinyo aina ya divai, kukaushwa kuwa zabibu kavu na mbegu zake huzalisha mafuta.

Kumbukumbu za kihistoria zinaeleza kwamba kilimo cha mizabibu kwa ajili ya uzalishaji wa zabibu kilianzia nchini Uturuki.

Misri, Ugiriki na Roma pia walilima zabibu kwa minajili ya kula na kutengeneza mvinyo. Ni kufuatia matumizi yake na faida kiafya, matunda haya yalisambaa Ulaya, Bara Afrika na Marekani.

Faida kiafya

Zabibu ni kiini kizuri cha fiber ambayo husaidia katika ukuaji wa viungo vya mwili, hasa kwa mtoto ambaye hajazaliwa. Pia matunda haya yameshamiri Vitamini, bila kusahau madini kama Potassium.

Wataalamu wa masuala ya afya wanasema zabibu ni miongoni mwa matunda yanayosaidia kudhibiti magonjwa mbalimbali kama; Saratani, Moyo, Pumu, shida za kutoona na kusokotwa na tumbo.

“Wanaougua Kisukari wanahimizwa kula zabibu kwa wingi. Kwa jumla hufai kukosa matunda kwenye ratiba yako ya lishe,” aeleza Mary Ann Njeri, mtaalamu wa afya.

Kenya, inaorodheshwa miongoni mwa mataifa bora ulimwenguni kukuza matunda haya kwa sababu ya hali bora ya anga.

Barani Afrika, Afrika Kusini ndiyo inaongoza.

Kiwango cha joto la wastani mchana, kijibaridi usiku na mchanga wenye virutubisho vya kutosha, pamoja mvua ya kadri maeneo mbalimbali nchini, ni baadhi tu ya vigezo vinavyoiweka Kenya katika ramani ya mataifa yanayofanikisha kilimo cha zabibu.

Mengi ya matunda haya huzalishwa Meru. Naivasha, Mandera, Kibwezi na Mombasa, pia ni maeneo yaliyotajwa kuwa bora katika kulima zabibu.

Licha ya Kajiado kushuhudia kiangazi mara kwa mara, kaunti hii ina uwezo kukuzwa matunda haya.

Eneo la Nkoroi, Ongata Rongai, katika shamba lenye ukubwa wa ekari tano, Agnes Omingo ametengea zabibu karibu thumuni ekari (1/8).

Agnes Omingo, mkulima wa eneo la Ongata Rongai kaunti ya Kajiado, aonyesha mzabibu uliozaa zabibu. Picha/ Sammy Waweru

Pembezoni ana shimo la maji na kidimbwi ambapo hutumia jenereta katika umwagiliaji wa mizabibu pamoja na miti ya matunda mengine.

“Nimefanikisha kulima matunda kwenye kiunga hiki kwa kutumia mfumo wa mifereji kunyunyizia mimea maji,” Bi Agnes ambaye pia ni mfugaji wa ng’ombe wa maziwa akaambia Taifa Leo wakati wa mahojiano katika shamba lake.

Upanzi

Zabibu ni miongoni mwa matunda rahisi mno kulima, ikiwa mkulima ana chanzo cha maji ya kutosha kila wakati.

“Kazi huwa kupogoa matawi (prunning), kunyunyizia maji na kuyatunza kwa pembejeo,” anasema.

Kitaalamu, shughuli ya kupogoa hupendekezwa ili mmea usalie na matawi yatakayoweza kutunzwa vyema.

Meshack Wachira, mtaalamu wa masuala ya kilimo anasema matawi yanapopogolewa, hupunguza ushindani wa lishe; maji na mbolea. Anaeleza kuwa hatua hii huwezesha mkulima kupata mazao bora na yenye soko.

“Matawi yasipopogolewa, mazao yapo ingawa ni madogo na ya hadhi ya chini. Kupata soko inakuwa kitendawili. Yaliyopogolewa huzalisha mazao bora, matunda yanakuwa makubwa, na yenye soko la haraka,” anafafanua mdau huyu.

Bi Agnes anasema upanzi wa mizabibu hauna ugumu wowote ule.

Anapendekeza kuyapanda kwenye mashimo, akishauri urefu wa shimo kuenda chini uwe inchi 12 na upana wa kipimo sawa na hicho.

Nafasi kutoka shimo moja hadi lingine iwe futi 6, na laini za mashimo ziwe na nafasi ya futi 10.

“Wakati wa upanzi, rejesha mchanga wa juu uliochimbwa uchanganywe na mbolea, ufikie inchi 4. Mwagilia maji shimoni, kisha upande mche wa mzabibu kwa umakinifu,” ashauri Agnes. Mizizi ifunikwe hadi inchi 6, inchi 2 zilizosalia kwa jumla ya 12 (urefu wa shimo kuenda chini) ni za kuitunza kwa maji na mbolea ya kisasa. Pia, nafasi hiyo hutumika kwa minajili ya kuweka nyasi za boji (mulching), ili kuzuia mnyauko wa maji hasa msimu wa kiangazi.

Mbegu bora

Bw Daniel Mwenda ambaye ni mtaalamu wa kilimo haswa matunda, anahimiza wanazaraa kupanda mbegu bora za zabibu.

“Kabla mkulima ang’oe nanga kupanda matunda haya, atafiti mbegu bora. Kuna mbegu nyingi sana bandia sokoni. Atapata zile bora kupitia wakulima waliofanikisha kilimo hiki na kupitia wataalamu wa kilimo,” ashauri.

Anaonya kuwa upandaji wa mbegu bandia ni mojawapo wa kiini cha mazao duni. Mbegu zilizoafikia ubora ni zilizoidhinishwa na tasisi ya kitaifa ya utafiti wa kilimo na ufugaji nchini (Karlo).

Ekari moja moja ina uwezo wa kusitiri zaidi ya mizabibu 2,000, washauri wa kilimo wakihoji kiasi hiki kinazalisha karibu tani 13, sawa na kilo 13,000.

Kilo moja ya zabibu nchini haipungui Sh60.

Changamoto katika ukuzaji wa zabibu ni athari za wadudu kama vidukari na Japanese Beetles.

Magonjwa yanayoshuhudiwa ni Powdery Mildew na Black Rot.

Kuyadhibiti, mkulima anahimizwa kupata ushauri kutoka kwa wataalamu wa zaraa ili kupendekezewa dawa bora.