Habari Mseto

Mizozo kuhusu mipaka yaendelea kusababisha mauti

October 3rd, 2019 2 min read

Na BENSON MATHEKA

MIZOZO kuhusu mipaka ya maeneo tofauti nchini imekuwa ikisababisha hasara kubwa huku watu wakiuawa, nyumba kuchomwa na mali ya mamilioni ya pesa kuharibiwa.

Katika visa vya hivi punde, ghasia zimeshuhudiwa kaunti ya Narok koo mbili zikizozania mpaka, katika mpaka wa kaunti za Kitui na Tana River na eneo na Banisa, Mandera kwenye mpaka wa Kenya na Ethiopia.

Katika muda wa wiki mbili, watu zaidi ya kumi wamepoteza maisha yao kwenye mizozo ya mipaka na ni hali ambayo huwa inajirudia mwaka baada ya mwaka.

Baadhi ya mizozo hiyo imedumu kwa miaka mingi na kuibua maswali kuhusu kujitolea kwa serikali kuimaliza.

Mnamo Jumatano, serikali ilichukua hatua ya kuweka alama mpaka kati ya koo mbili zinazopigana kaunti ndogo ya Trans Mara, kaunti ya Narok. Koo za Siria na Iruasin Gishu zimekuwa zikipigania mpaka wa Nkararo- Enooretet ambapo watu wawili waliuawa wiki jana.

Ghasia zimekuwa zikitokea katika mpaka huo kila mwaka tangu 1997 watu wapatao 50 walipouawa. Mnamo 2017, watu 9 waliuawa ghasia zilipozuka eneo hilo kuhusiana na mpaka.

Serikali ilichukua hatua ya kuweka alama mpaka huo ghasia zilipozuka majuzi na washukiwa kadha, akiwemo chifu kukamatwa.

Mzozo umekuwa ukishuhudiwa eneo hilo kati ya jamii za Wakisii na Wamaasai ambapo watu wamekuwa wakiuawa, mashamba kuchomwa na mifugo kuibwa au kuuawa.

Hali ya taharuki ingali imetanda katika mpaka wa kaunti ya Kitui na Tana River baada ya watu watatu kuuawa wiki mbili zilizopita.

Mamia ya wakazi wa Kitui walitoroka makwao wakihofia kushambuliwa na majangili wanaodaiwa kutoka kaunti jirani.

Juhudi za viongozi wa eneo hilo kutatua mzozo huo zimegonga mwamba licha ya maafisa wakuu wa serikali kutembelea eneo hilo.

Hali ni kama hiyo katika mpaka wa Isiolo na Meru ambapo ghasia zimekuwa zikitokea mara kwa mara. Watu 10 waliuawa kwenye ghasia kuhusu mpaka huo 2017.

Kupigania raslimali

Kulingana na shirika la Msalaba Mwekundu nchini, ghasia nyingi hutokea wakazi wakipigania rasilimali kama vile ardhi, maji na malisho.

Imekuwa na kawaida kwa ghasia kutokea katika mpaka wa kaunti za Baringo na Turkana hasa eneo la Kapendo. Watu zaidi ya 160 wakiwemo maafisa wa polisi wameuawa eneo hilo tangu 2015.

Juhudi za viongozi wa eneo hilo za kutafuta amani zimelifanya kushuhudia utulivu kiasi katika kipindi cha miezi sita iliyopita.

Mbali na usalama kudorora katika mipaka ya maeneo ya humu nchini, Wakenya wamekuwa wakihangaishwa na wahalifu kutoka mataifa ya kigeni hasa katika mipaka ya Kenya na Somalia, Ethiopia na Uganda.