Mizozo ya uwaniaji vyeo yatishia umoja wa ‘Kenya Kwanza’

Mizozo ya uwaniaji vyeo yatishia umoja wa ‘Kenya Kwanza’

Na LEONARD ONYANGO

MVUTANO wa ugavana ndani ya muungano wa ‘Kenya Kwanza’ ulidhihirika Jumanne baada ya Seneta wa Nairobi, Johnson Sakaja na Mhubiri Margaret Wanjiru kurushiana cheche za maneno hadharani.

Bi Wanjiru amekuwa akipigiwa debe na Naibu wa Rais Ruto kuwania ugavana wa Nairobi kupitia chama cha United Democratic Alliance (UDA).

Lakini hatua ya kinara wa Amani National Congress (ANC) Musalia Mudavadi kuungana na Dkt Ruto chini ya muungano wa ‘Kenya Kwanza’ inaonekana kuharibu hesabu za Bi Wanjiru.

Kulingana na duru, upande wa Bw Mudavadi unataka uachiwe ugavana wa Nairobi kutoa mwanya kwa Seneta Sakaja kupeperusha bendera ya muungano wa Kenya Kwanza.

Bw Sakaja, ambaye alichaguliwa kupitia Jubilee mnamo 2017, anatarajiwa kuhama chama hicho kinachoongozwa na Rais Uhuru Kenyatta na kujiunga rasmi na ANC.

Wawili hao walirushiana cheche za maneno mbele ya Bw Mudavadi na kiongozi wa Ford Kenya Moses Wetang’ula katika mkutano wa kisiasa uliofanyika katika eneo la City Park mtaani Parklands, Nairobi.

Bi Wanjiru alikuwa akihutubia mamia ya watu waliofika kwenye mkutano huo kabla ya kuanza kuzozana na Bw Sakaja ambaye alikuwa akiteua wanasiasa wanaohutubu.

Bi Wanjiru alikerwa na hatua ya Bw Sakaja kukatisha hotuba yake kabla ya kumaliza kujipigia debe kwa wapigakura alipochukua kipaza sauti kwa nguvu kutoka kwake, hatua iliyomkera mbunge huyo wa zamani wa Starehe.

Seneta huyo wa Nairobi alimtaka Bi Wanjiru kukatiza hotuba yake baada ya kundi la vijana kuanza kupiga kelele.Baadaye, Bw Sakaja alishutumu vijana hao akidai kuwa walimwaibisha akiwa seneta wao.

“Mmeniaibisha sana. Sisi kama ‘Kenya Kwanza’ tunafaa kumpa kila mmoja wetu nafasi ya kujieleza. Unapokasirishwa na muziki unaochezwa redioni hauharibu redio, bali unabadilisha stesheni,” akasema Bw Sakaja.

You can share this post!

Serikali kutoa vibali vya kazi kwa wataalamu wa tiba za...

Mwingine afungwa miaka 24 jela kwa ufisadi

T L