Mizozo ya wanasiasa yaua ziara ya Uhuru Ukambani

Mizozo ya wanasiasa yaua ziara ya Uhuru Ukambani

Na CHARLES WASONGA

RAIS Uhuru Kenyatta ameahirisha ziara yake ya siku mbili eneo la Ukambani kwa kile ambacho Ikulu ilisema ni hofu ya kueneza virusi vya corona.

Hata hivyo, duru zilisema ziara hiyo amiliyoratibiwa kwanza leo, ilifutiliwa mbali kutokana na mivutano miongoni mwa viongozi wa Ukambani.

Pia viongozi hao walikuwa wametofautiana kuhusu maeneo ambako Rais Kenyatta angezuru na miradi atakayozindua.

‘Ziara hii imeahirishwa kwa sababu hatujaonyesha umoja wakati wa maandalizi yake. Tofauti hizi zinachochewa na baadhi ya wanasiasa ambao hawakuwa katika Ikulu ya Nairobi tulipokutana na Rais,’ Mbunge mmoja kutoka eneo hilo ambaye aliomba kutotajwa jina alisema jana.

Hata hivyo, kumekuwa na mgawanyiko kuhusu ziara hiyo miongoni mwa makundi mawili ya viongozi wa Ukambani.

Wao ni wanasiasa wanaoegemea mrengo wa kiongozi wa Wiper, Bw Kalonzo Musyoka na wale wanaounga mkono muungano wa kiuchumi wa Ukanda wa Kusini Mashariki mwa Kenya (SEKEB).

Wakati wa ziara hiyo, Rais Kenyatta alipangiwa kuzuru kaunti za Machakos, Makueni na Kitui. Makueni, kiongozi wa taifa alipangiwa kuzuru jiji la kiteknolojia la Konza kabla ya kukagua ujenzi wa bwawa la Thwake.

Baadaye angeongoza hafla ya uzinduzi wa barabara ya Kibwezi kwenda Kitui.Rais Kenyatta pia alikuwa ameratibiwa kukagua miradi kadhaa ya maendeleo katika kile wadadisi walisema ni kukita ushawishi wake kisiasa katika eneo hilo.

Mnamo Jumapili, Gavana wa Machakos Alfred Mutua alisema wao kama viongozi wa Ukambani wanamkaribisha Rais Kenyatta katika eneo hilo kwa matarajio ya ‘kuvuna’ maendeleo kutoka serikali kuu.

‘Tunamkaribisha Kiongozi wa Taifa kwa matarajio kwamba ziara yake italeta matunda katika eneo letu. Vile vile, hatutarajii kuwa wanasiasa wasio na kazi watatumia nafasi hiyo ili kuonekena wakitembea na Rais,’ akasema.

‘Hii ni nafasi bora kwa Rais kujionea mwenyewe changamoto ambazo zinatukumba hapa Ukumbani ili atusaidie kuzikabili chini ya muungano wa kiuchumi wa SEKEB. Ningeomba aongeze ziara hiyo ili idumu kwa siku tatu,’ akaongeza Dkt Mutua.

Mnamo Juni 25, Rais Kenyatta alizuru kaunti ya Kitui ambapo alizindua Kanisa Katoliki la Mariam Shrine of Our Lady of Protection katika eneo la Museve.

You can share this post!

Tofauti zaibuka kuhusu uteuzi Kadhi wa kike

Wabunge watisha kumtimua Magoha