HabariSiasa

Mjadala bungeni kuhusu mayai milioni 33 kutoka Uchina

March 14th, 2019 1 min read

Na PETER MBURU

UFICHUZI wa Wizara ya Kilimo kuwa kampuni za ujenzi za Uchina zinaingiza nchini mamilioni ya mayai, Alhamisi ulizua mjadala mkali kwenye kikao cha Kamati ya Bunge kuhusu Kilimo.

Ilibainika kuwa katika kipindi cha miaka miwili, zaidi ya mayai milioni 33 yameingizwa nchini kutoka Uchina.

Serikali imekuwa ikiruhusu kampuni za uchina ambazo zimepewa kandarasi za kutengeneza barabara kuingiza mayai nchini.

Kulingana na ripoti hiyo ya wizara, mnamo 2017, Kenya iliingiza mayai milioni 15 kutoka mataifa mbalimbali ya kuanguliwa vifaranga na kuliwa.

Mayai yote ya kuliwa yalitoka Uchina, yakiingizwa na kampuni za Sinohydro Corporation Ltd, Chia Town Supermarket Ltd, Seven Days International (K) Ltd na Ling Yue International CO Ltd.

Ripoti hiyo ilizua mjadala mkali miongoni mwa wabunge, ambao walishangaa sababu ya serikali kuruhusu mayai kuingizwa kutoka nje, wakati tayari kuna mayai ya kutosha Kenya.

Wanachama wa Kamati ya Bunge kuhusu Kilimo wakiwa katika kikao na maafisa kutoka Wizara ya Kilimo, kuwauliza maswali Februari 14, 2019. Picha/Peter Mburu

“Iweje serikali inaruhusu mayai kuingizwa nchini wakati yako ya kutosha? Sharti serikali iwalinde wakulima kutokana na hali hii ambayo inawanyima soko la chakula hiki,” akasema mwenyekiti wa kamati hiyo Adan Haji.

Alitaka Wizara ya Kilimo iandikie mamlaka zote zinazohusika kusitisha kabisa kuingizwa kwa mayai kutoka mataifa yasiyo ya muungano wa Comesa.

Waziri Msaidizi wa Kilimo, Bw Andrew Tuimur alilaumu mamlaka Ubora wa Bidhaa (KEBS) na Idara ya Afya ya Umma kwa kuruhusu uingizaji wa mayai hayo bila kuhusisha wizara.

Waziri alisema wameruhusu asilimia ndogo ya mayai kuingizwa, lakini kiwango kikubwa kimeruhuswa na idara zingine.

Wafugaji wa kuku wa mayai nchini wamekuwa wakilalamika kwa kukosa soko la bidhaa hiyo, kutokana na kufurika kwa mayai kutoka nje ya nchi.