Makala

MJADALA: Je, ni vyema mwanamke kubugia pombe?

May 29th, 2019 2 min read

Na MWANGI MUIRURI

ROSE Muriithi ambaye ni mtaalamu wa masuala ya kijamii anasisitiza kuwa hakuna shida na mwanamke kubugia pombe, bora tu aithibiti asije akazama ndani ya ulevi kiholela.

Anasema kuwa ukiwa wewe ni mwanamke wa kujitegemea, uko na pato lako na majukumu yako ya kujenga maisha yako na taifa, basi unaweza ukiamua, ukawa wa kunywa angalau chupa tatu kwa wiki au glasi kadhaa kwa wiki hiyo za mivinyo ya matunda.

Anasema kuwa kile ambacho atakukanya kushiriki ukiwa mwanamke ni tabia ya ombaomba pombe katika mabaa kwa kuwa hilo ni sawa na kuwa sumbua na ambapo

maadili yako yatatiliwa shaka.

“Chukua mfano kama wangu. Mimi niko na kazi yangu na pia niko na biashara zangu. Sina bwana na sio kwa kuwa sijapata wa kunichumbia, bali ni vile nimeamua kuwa maisha yangu yako na utulivu kamili nikiwa sijaolewa,” asema.

Anasema kuwa ako na watoto wawili ambao wanasoma katika shule za kibinafsi na katika harakati zake za kusaka raha ya kimaisha, huwa anatua katika baa hapa na pale, na kujinunulia chupa zake tatu au glasi kadhaa za mvinyo wa matunda.

“Mfano huo nimekupa ndio uangazie masuala kadhaa: Niko na kazi, sina bwana na majukumu ya malezi ninayo. Ikiwa hayo yote hayakwami, mbona nisijiamulie aina yangu ya raha?” ahoji.

Anasema kuwa ule msimamo wa kimila kuwa wanawake wasije wakafikiria kuwa wa kujisimamia bali wawe chini ya amri ya mume au jamii mashinani umepitwa na wakati kwa kuwa leo hii, hii ni dunia ya usawa wa kijinsia.

Bi Rose Muriithi akiwa katika baa ya Empire, mjini Murang’a. Picha/ Mwangi Muiruri

“Lakini ukiwa umeolewa, na bwanako hajakupa idhini au pesa za kunywa pombe, kaa nyumbani. Ulijituma kuwa chini ya amri ya bwanako na ni lazima utii ikiwa haja yako ni kujenga familia yako. Ikiwa bwana huyo amekupa idhini ya kunywa pombe, hakikisha mnaandamana naye kwa kuwa ni maisha magumu kwa mwanamke akitangamana na walevi wengine ndani ya baa,” asema.

Anasema kuwa sio mara moja ameingia katika baa na kubebwa na wanaume walevi kama kahaba na kuanza kuchumbiwa kwa msingi wa ngono.

“Lakini kujitegemea kwangu huwa kunawapa taswira nyingine kwa kuwa huwa najiunga nao, nitanunua nao wanunue na iwe kwamba tuko kwa ulevi kwa usawa wala sio kana kwamba nimeingia hapo kusaka pombe ya msaada,” asema.

Anasema kuwa nidhamu yake ndani ya baa ni kuwa, hawezi akazidisha saa mbili akilewa na hawezi akapitisha kiwango cha chupa tatu.

“Nikishatimiza haja yangu ndani ya baa, nitatoka, niingie kwa gari langu na kisha nijitoe mahali hapo na niende moja kwa moja hadi kwa nyumba yangu ambapo mimi ndio hupika chakula changu na cha familia,” asema.

Anaonya wanawake kuwa pombe ni mbaya tu ikiwa huna adabu ya kudhibiti kiwango cha ulevi na uishie kuwa mlevi wa kiholela, uwe na nidhamu ya kujua pombe yako ni gani wala sio kubugia kila aina ya takataka ndani ya soko na hatimaye, uwajibikie majukumu na mito yako ya kimaisha.

Anasema kuwa wanawake walio katika ndoa sio vyema wajiingize katika maisha ya ulevi wa kusaka utulivu wa moyo, lakini ikiwa watapata ruhusa ya mabwana zao, “kujeni nitawaonyesha ustaarabu wa ulevi kwa kuwa niko na tajiriba ya miaka minane sasa.”