Mjadala wapamba moto kuhusu vyakula vya GMO

Mjadala wapamba moto kuhusu vyakula vya GMO

WINNIE ONYANDO Na BENSON MATHEKA

TANGAZO la hivi majuzi la serikali kuondoa marufuku yaliyowekwa dhidi ya uzalishaji, uagizaji na uuzaji wa vyakula vilivyokuzwa kisayansi, maarufu GMO, limezua hisia na mjadala mkali nchini.

Serikali ilisema kwamba, hatua hiyo inalenga kuimarisha utoshelevu wa chakula ili kulinda maelfu ya Wakenya wanaokumbwa na njaa.

Japo serikali na watafiti wa kilimo wanasema kuwa, uchunguzi uliofanywa kuhusu vyakula vya GMO ulionyesha kuwa vyakula hivyo ni salama kwa matumizi ya binadamu, wanaharakati mbalimbali bado wanashikilia kuwa GMO ni hatari kwa afya ya mwanadamu.

Bw Timothy Njagi, mtafiti katika Taasisi ya Tegemeo yenye makao yake katika Chuo Kikuu cha Egerton, alisema kuwa uamuzi huo ulicheleweshwa kwa muda mrefu na kuondolewa kwake kutasaidia nchi kujitosheleza kwa chakula.

“Mahindi ya GMO ni ya bei nafuu kuliko yale ya kawaida na tukianza kuagiza kutoka nje ya nchi, yatapunguza gharama ya chakula nchini,” akasema Dkt Njagi.

Kadhalika, alisema hatua hiyo pia itasaidia katika kukabiliana na gharama kubwa ya vyakula vya mifugo, ambavyo kwa miaka mitatu iliyopita imekuwa ya juu.

Kwa upande wake, Dkt Roy Mugiira, afisa mkuu mtendaji wa Mamlaka ya Taifa ya Usalama wa Biolojia, inayodhibiti sekta hiyo alikaribisha hatua hiyo akisema itapunguza gharama ya maisha nchini.

“Katika siku chache zijazo, sasa tutatoa miongozo ya kufuatwa katika kuagiza au kukuza aina hizi, lakini ninaweza kusema kuwa, sasa ni halali kuwa na mazao ya GMO nchini,” alisema Dkt Mugiira.

Hata hivyo, utafiti kutoka nchi ya Ufaransa ulibainisha kuwa vyakula vya GMO husababisha maradhi ya kansa.

Vyakula vya GMO vilipigwa marufuku Kenya mnamo Novemba 2012 wakati wa utawala wa Rais wa zamani Mwai Kibaki.

Hatua hiyo ilifuatia utafiti uliohusisha vyakula vya GMO na kansa na ambao wanaharakati wanatumia kukosoa uamuzi wa hivi majuzi wa serikali.

Wanaharakati wanasema kwamba, hatua ya serikali ya kuondoa marufuku hiyo ilifanywa kwa pupa na inaweza kuweka afya ya Wakenya kwenye hatari.

“Uamuzi wa haraka wa kuondoa marufuku ya kuingiza nchini GMO ulioruhusu pia ukuzaji vyakula hivyo ulifanywa bila kushirikisha umma,” makundi ya wanaharakati yalisema kwenye taarifa ya pamoja Alhamisi.

Yalisema kwamba, utoshevu wa chakula sio tu wingi wake lakini pia ubora wake.

Utafiti wa Ufaransa ulionyesha kuwa, panya waliotumiwa katika utafiti huo walipatikana na ugonjwa wa kansa.

Utafiti huo pia ulionyesha kwamba, uhandisi wa biokemikali ungeleta hatari za kiafya kwa wanadamu pia.

Ilibainishwa kuwa vyakula va GMO huleta athari kwa mazingira.Kadhalika, ilibainishwa kuwa, kampuni zinazozalisha vyakula hivyo haziaminiki.

Hata hivyo, mnamo Desemba 2019, Kenya iliidhinisha kilimo cha pamba ya GMO baada ya miaka mitano ya majaribio ya shambani.

Kufuatia kuondolewa kwa marufuku hiyo, Kenya sasa inajiunga na orodha ya nchi za Afrika zinazolima mazao ya GMO ambazo ni pamoja na Nigeria, Afrika Kusini, Ethiopia na Malawi.

Katika muungano wa Ulaya nchi za Ufaransa, Ujerumani, Austria, Ugiriki, Hungary, Uholanzi,Lativia,, Lithuania, Luxembourg, Bulgaria, Poland, Denmark, Malta, Slovenia, Italia Croatia zimepiga marufuku bidhaa za GMO.

Katika bara la Asia, Uturuki, Kyrgyzstan, Bhutan na Saudi Arabia haziruhusu GMO sawa na Belize, Ecuador, Peru na Venezuela katika kusini mwa Amerika ambazo zimepiga marufuku vyakula hivyo kulinda mazingira na afya.

Amerika, haina sheria rasmi ya kupinga marufuku GMO, kulingana na ripoti ya worldpopulationreview ya mwaka huu.

  • Tags

You can share this post!

Mhariri wa KBC apata afueni kesi ya kusukumwa jela

Polisi wanasa mwanamume akiuza risasi

T L