Habari Mseto

Mjakazi hofu tele pacha wake watakosa elimu ya sekondari

December 18th, 2019 1 min read

Na SAMMY KIMATU

PACHA waliofanya Mtihani wa Kitaifa wa Shule za Msingi (KCPE) mwaka uliopita, wanahofia kukosa kujiunga na Kidato cha Kwanza kwa kukosa karo.

Mama yao, Bi Gladys Wangui, 39, hufanya kazi za nyumbani na hivyo basi, anasongwa na mawazo kuhusu atakapopata karo na pesa za matumizi kuwezesha watoto hao kuendeleza masomo yao bila matatizo.

Familia hiyo hutoka katika kijiji cha Miteru kilichoko tarafani Endarasha, Kieni Kusini katika Kaunti ya Nyeri lakini Bi Wangui hufanya kati katika maeneo ya Toll, Juja, Kaunti ya Kiambu.

“Kusema kweli mshahara wangu hauwezi kukimu mahitaji,” akasema wakati wa mahojiano jana katika Jumba la Nation Centre, jijini Nairobi.

Pacha hao ni Evaline Wanjiru na Sharon Wangari wenye umri wa miaka 14. Wawili hao walisomea katika Shule ya Msingi ya Mitero eneo la Kieni.

Baada ya matokea ya KCPE 2019 kutolewa, Evaline alipata alama 299 huku Sharon akizoa alama 325. Makubwa ni kwamba licha ya tofauti za alama alama zao, wote wawili wamechaguliwa kujiunga na Shule ya Upili ya Othaya Girls.

Mama yao alieleza kwamba kutokana na mzozo wa nyumbani, alitalikiana na mumewe kwa hivyo yeye ndiye tegemeo lao kimaisha.

Kando na pacha hao, ana mtoto mwingine wa kiume ambaye ana matatizo ya akili lakini huyo alibaki na mumewe wa zamani kwa vile, kulingana naye, ni mwiko mama kuondoka na mtoto wa kiume anapotalikiana na mumewe.