Habari Mseto

Mjane wa Cohen aomba korti imruhusu atwae vya kwake

November 14th, 2019 1 min read

Na Richard Munguti

MJANE wa bwanyenye Tob Cohen, Sarah Wairimu Kamotho, anayeshtakiwa kwa mauaji ya mumewe pamoja na mfanyabiashara Peter Karanja amewasilisha ombi katika mahakama kuu aruhusiwe kurudi katika makazi yake eneo la Lower Kabete, Nairobi.

Makazi ya Sarah yaliwekwa chini ya ulinzi wa maafisa wa Polisi tangu maiti ya Cohen ilipokutwa imetupwa ndani ya tangi la maji.

Katika ombi lililowasilishwa na wakili Philip Murgor, Sarah ameomba korti imkubalie arudi katika makazi yake kutwaa mbwa wake wawili anaowatambua kwa majina Major na Snow.

Mbali na mbwa hao anaodai walipelekwa mahala asiojua na Polisi Sarah anaomba korti imwamuru Mkurugenzi wa Uchunguzi wa Jinai (DCI) George Kinoti arudishe gari lake alililochukua.

“Naomba hii mahakama imwamuru DCI anirudishie gari langu niwe nikitumia kushughulikia mahitaji yangu ya usafiri,” asema Sarah.

Pia ameeleza katika ombi alilowasilisha mbele ya naibu wa msajili wa mahakama kuu anataka kuchukua viatu, vipodozi, mikoba na nguo mbali na redio na CDs.

Sarah ameomba korti imwamuru DCI afunike viti vilivyoko katika makazi yake visipate vumbi jingi na kuchukua vifaa vya kucheza Golf.Mshtakiwa huyu wa mauaji ya mfanyabiashara huyu mtajika kutoka Uholanzi anaomba aruhusiwe kuchukua vikombe kutoka jikoni na mvinyo na vyakula mbali mbali.

“Mshtakiwa anataka kuchukua jenerata muundo wa Honda na nguo kwa vile amelazimika kununua nguo mpya. Anategemea msaada wa marafiki na nguo zake zimefungiwa ndani ya nyumba iliyo chini ya ulinzi wa Polisi,” asema Murgor.

Pia anataka aruhusiwe aondoe televisheni picha, filamu, redio ,santuri na vitabu mbali mbali.“Mshtakiwa hana mapato sasa kwa vile aliamriwa na mahakama asiende kwa biashara za mumewe.Anategemea marafiki kupata pesa za kufika mahakamani kila wakati,” asema Murgor.

Amedai DCI hajampa nakala ya vifaa alivyotoa kwa nyumba yake katika uchunguzi unaoendelea.Sarah na Karanja wameshtakiwa kumuua Cohen mnamo Julai 19/20 2019.