Habari

Mjane wa Simon Mukuha afariki wiki tatu baada ya mumewe kuzikwa

September 17th, 2019 1 min read

Na SIMON CIURI

MONICAH Wanjiru, mjane wa mwenyekiti wa Naivas, Simon Mukuha, amefariki kutokana na kansa hospitalini Aga Khan, wiki tatu tu baada ya mumewe kuzikwa.

Wanjiru ameaga dunia akiwa na umri wa miaka 58.

Kifo chake kimetokea katika kipindi cha muda wa wiki tatu tu tangu mumewe azikwe Agosti 29, 2019, katika makaburi ya Langata, Nairobi.

Vyanzo vimeambia Taifa Leo kwamba Wanjiru amekuwa akiugua saratani kwa muda mrefu, ambapo wakati wa uhai wa wanandoa hawa, Mukuha aliwahi kumpeleka nchini India ili akatibiwe.

Hata hivyo, iligundulika kansa ilikuwa imeenea sana na kufikia hatua ya ukomavu kiasi kwamba wataalamu wa afya walishauri arudishwe nyumbani kisha awe akipewa matibabu na matunzo ya kina kutoka kwa wataalamu.

Marehemu alikuwa amelazwa katika chumba cha uangalizi maalum katika hospitali ya Aga Khan majuma mawili yaliyopita baada ya hali yake ya afya kudhoofika, kulingana na Meneja Mkurugenzi wa Naivas, Bw David Kimani.

Kimani amesema mwili wa marehemu Wanjiru utazikwa Alhamisi eneo la Langata ambapo kaburi lake litakuwa karibu na la mumewe.