Habari Mseto

Mjarabu wa kitaifa waanza kwa wanafunzi wa Gredi ya Nne na Darasa la Nane

October 21st, 2020 1 min read

Wanafunzi wa Donholm Catholic Primary, Nairobi wakifanyia mjarabu wa Mitihani wa Darasa la Nane mnamo Oktoba 21, 2020. Picha/Chris Adungo

Na CHRIS ADUNGO

WANAFUNZI wa Darasa la Nane na Gredi ya Nne kote nchini Jumatano walianza kufanya mitihani ili kubaini uthabiti wa kumbukumbu zao katika masomo baada ya kuwa nyumbani kwa miezi sita.

Baraza la Mitihani nchini (KNEC), limeitaja mitihani hiyo kuwa mijarabu ya kupima na kubaini utayari wa wanafunzi hao kuendelea na masomo baada ya kuwa nyumbani kwa kipindi kirefu kutokana na janga la corona. Hata hivyo, shule nyingi zilikabiliwa na changamoto za kupata karatasi za mitihani hiyo kutoka kwa tovuti ya KNEC.

Mitihani hiyo iliyokuwa ianze Oktoba 19, 2020 iliahirishwa hadi Oktoba 21 ili kupisha maadhimisho ya Mashujaa Dei yaliyoongozwa na Rais Uhuru Kenyatta katika uwanja wa Gusii, Kaunti ya Kisii.

Kwa mujibu wa Ratiba ya KNEC, wanafunzi wa Gredi ya Nne watafanya mitihani hiyo kwa siku nne huku wa Darasa la Nane wakikamilisha mijarabu yao kwa siku tatu.

Katika siku ya kwanza, wanafunzi wa Gredi ya Nne walitahiniwa katika stadi za Kuzungumza na Kusoma kwa Sauti kwenye somo la Kiingereza. Kila mtahiniwa alihitajika kufanya hivyo kwa dakika 10 mbele ya mwalimu wa somo lake.

Wanafunzi wa mahitaji maalum, hasa wanaotumia breli, na wasio na uwezo wa kusikia pia walishirikishwa kwenye mitihani hiyo chini ya uelekezi wa walimu wao.

Katika siku ya pili, (Oktoba 22), wanafunzi watatahiniwa kuhusu stadi ya Ufahamu, Kusoma na Kuandika kwenye somo la Kiingereza kwa muda wa saa moja na dakika 20.

Watahiniwa hao wa Gredi ya Nne watafanya pia mitihani katika masomo ya Mazingira, Sayansi na Teknolojia.

Wanafunzi wa Darasa la Nane walianza mijarabu yao kwa kufanya mtihani wa Hisabati, Kiingereza na Insha ya Kiingereza mnamo Oktoba 21. Wamepangiwa kufanya mitihani katika masomo ya Sayansi, Kiswahili na Insha ya Kiswahili mnamo Oktoba 22 kisha masomo ya Jamii na Dini mnamo Oktoba 23.