Michezo

Mjeledi wa FIFA wachapa, mataifa yatozwa mamilioni

October 11th, 2019 2 min read

Na MASHIRIKA

SHIRIKISHO la Soka Duniani (FIFA) limetoza mashirikisho ya soka ya Hong Kong, Indonesia, Sierra Leone na Sudan jumla ya faini ya Sh14.4 milioni kwa utovu wa nidhamu wa mashabiki wao wakati wa mechi za kufuzu kushiriki Kombe la Dunia la mwaka 2022.

Hong Kong italipa Sh1.5 milioni baada ya mashabiki wake kukosa heshima wimbo wa taifa wa China ukichezwa kabla ya mechi kati ya Hong Kong na Iran mnamo Septemba 10.

Mashabiki wa Hong Kong walipiga kelele kukejeli wimbo huo uwanjani Hong Kong.

Mechi hiyo iliandaliwa maandamano ya kupigania demokrasia yakiwa yamechacha dhidi ya utawala wa Uchina katika eneo la Hong Kong, ambalo lilitawaliwa na Uingereza hadi mwaka 1997.

FIFA ilisema Jumatano kuwa faini dhidi ya Hong Kong ni adhabu ya “kufanya usumbufu wakati wa nyimbo za taifa zinachezwa na kutumia vifaa kupeperusha ujumbe ambao haufai katika michezo”.

Mechi ijayo ya Hong Kong, ambayo ilipoteza 2-0 dhidi ya Iran, itakuwa dhidi ya Bahrain uwanjani humo mnamo Novemba 14.

Indonesia imetozwa faini ya Sh4.6 milioni kwa usumbufu wa mashabiki wake ilipoalika majirani Malaysia.

Mchuano huo ulisimamishwa kwa dakika kadhaa katika dakika za lala-salama kwa sababu ya makabiliano ya mashabiki. Malaysia iliibuka mshindi kwa mabao 3-2 ikipata bao la ushindi dakika saba baada ya muda wa kawaida kukamilika.

Malaysia yaonywa

Kwa mara ya kwanza, FIFA pia ilionya Malaysia kwa mashabiki wake kukosa nidhamu na kutupa vifaa, na tena kwa kukosa mpangilio uwanjani mwake ilipoalika timu ya Milki za Kiarabu kwa mechi nyingine ya kufuzu siku chache baadaye.

Baada ya usumbufu wa mashabiki katika mechi ya nyumbani ya Sierra Leone dhidi ya Liberia mwezi Septemba, FIFA ilitangaza faini ya Sh5.2 milioni na kuamrisha Sierra Leone icheze bila mashabiki katika mechi yake ijayo ya nyumbani.

Sierra Leone ilibanduliwa nje ya mechi za kufuzu kushiriki Kombe la Dunia nchini Qatar kwa hivyo adhabu hiyo itatumikiwa wakati wa mechi ya kuingia Kombe la Afrika (AFCON) la mwaka 2021.

Sudan ilipigwa faini ya Sh3.1 milioni baada ya mashabiki wake kuingia uwanjani timu yao ikichuana na Chad.