Makala

Mji ambao ni ngome ya vijana wenye nywele chafu za rasta

April 8th, 2024 2 min read

NA MWANGI MUIRURI

KWA wageni ambao wameshawahi kutembelea mji wa Mukuyu, ulioko viungani mwa Mji wa Murang’a watakiri kwamba vijana wengi mtaani huwa na nywele za rasta ambazo ni chafu.

Nywele hizo ndizo katika siku za hivi karibuni zimekuwa nembo ya mtaa huo, zikiupa taswira ya kijambazi.

Mji wa Murang’a unasifika kwa kukumbwa mara kwa mara na uhalifu wa vijana wadogo ambao hujiita Gaza na ambao hushirikisha visa vya mashambulizi, mauaji, ubakaji na pia ulanguzi wa mihadarati.

Vijana hao huwa wameteka nyara mitaa kadha ya viunga vya mtaa wa Mukuyu na hatimaye kutumia baadhi ya maeneo ya mtaa huo kama ngome kushirikisha ukora hadi katikati mwa mji wa Murang’a ambao ndio makao makuu ya Kaunti.

Ni mji ambao aliyekuwa Kamishna wa Murang’a 2022 Bw Karuku Ngumo alikuwa ameutaja kama changamoto kwa usalama wa eneo hilo akisema “mitaa ya Majoyce, Maragi na Mjini ambayo yako viungani mwa Mukuyu lilikuwa limegeuzwa kuwa ngome za wahalifu”.

Sio mara moja ambapo wakazi wa Mji wa Mukuyu wamejitokeza katika vyombo vya habari wakiteta kuhusu uwepo wa vijana hao wa rasta chafuchafu kuwa hatari kwa usalama wao, wakionya kuchukua sheria mikononi mwao iwapo polisi hawatawawajibikia.

Cha kusikitisha wengi ni kwamba serikali huwa na udhaifu kuokota taka za mji huo hivyo basi kufanya rasta hizo kuonekana mbaya zaidi kwa kuwa katika pia mazingara ya taka kutapakaa.

Kwa sasa, mshirikishi wa muungano wa wafanyabiashara Murang’a Mashariki, Bw James Gita anasema kwamba “kunafaa kuwe na sheria vijana ambao nywele zao zitaonekana kuwa chafu washurutishwe kuzinyoa au kuziosha”.

Anasema kwamba “baadhi ya vijana hao huwa na rasta ambazo hazina afya kamwe na huwa kama hifadhi ya wadudu waharibifu na wa kufyonza damu”.

Alisema wengine huwa na sura za kutisha na wakiongeza uchafu wa mavazi na mwili, wanajiangazia tu kama hatari kwa maisha na mali ya majirani.

Alisema kwamba hali haijapewa heshima na ukweli kwamba baadhi ya wengi wa vijana ambao hunaswa katika visa vya uhalifu na pia kuwa watukutu wa sekta ya bodaboda nih ao hao tu wa nywele za rasta.

“Mimi nilifika katika mji huo wa Mukuyu ambapo kuna mrembo alikuwa amenipea deti. Akaniambia tukutane katika baa moja ya mji huo karibu na soko. Lakini katika kipindi cha dakika kumi, baa hilo ilikuwa imeingia vijana wembamba zaidi ya 20 walio na nywele za rasta nikaogopa,” asema msanii wa nyimbo za ushauri, Bw Kim wa Njoki.

Anasema kwamba aliingiwa na hofu huenda alikuwa amealikwa na mrembo huyo ili atekelezewe maangamizi “na ndipo hata sikumngojea afike ila tu nilihepa nikarudi Mjini Thika”.

Nywele za rasta katika jamii ya Agikuyu huhusishwa sanasana na harakati za vita vya ukombozi wa nchi kutoka kwa Wabeberu, kundi haramu la Mungiki, wakora na wavutaji bangi.

Hata hivyo, katika siku za hivi karibuni zimeanza kuhusishwa na wasanii.

Seneta wa Murang’a Bw Joe Nyutu anateta kwamba nywele za rasta katika siku za kisasa ni fashoni sawa na nyingine na hazifai kuwekwa chini ya shinikizo za shaka.

Hata hivyo, Bw Nyutu aliteta kwamba “ni lazima wenye nywele hizo wadumishe usafi na walizo nazo pia wajiepushe na uraibu wa mihadarati na ulevi kiholela”.

Anasema kwamba vijana wa kiume ndio wameathirika zaidi na ufugaji wa rasta chafu na ambazo hutoa taswira ya ukora kwa kuwa baadhi yao huvuta bangi, sigara, hutafuna miraa na ni walevi.

Alisema taswira hiyo huwa ni ya kufedhehesha na hata huchochea maafisa wa polisi kukamata wanaume walio na rasta kwa msingi kwamba ni wahalifu.

“Vijana hao wa Rasta mjini Mukuyu wanafaa wajiweke kwa kundi la kushauriana ili kujiosha nembo ya wanaotaka kuwaharibia sifa. Wasisitize kwamba wanachama katika muungano wao ni lazima wawe safi na wasio na mwingilio wa ujambazi,” akasema.

[email protected]