Habari Mseto

Mji wa Thika wasafishwa na kunyunyizwa kuepuka Covid-19

April 29th, 2020 2 min read

Na LAWRENCE ONGARO

IDARA ya Afya ya Umma kaunti ndogo ya Thika, Kaunti ya Kiambu, ilipuliza dawa mjini Thika na maeneo ya karibu katika vita dhidi ya coronavirus.

Shughuli hiyo ilifanyika Jumatatu katika maeneo tofauti huku wakazi wa Thika na wafanyabiashara wakipongeza hatua hiyo.

Mnamo mwishoni kwa wiki wakati Gavana wa Kiambu Dkt James Nyoro alizuru mjini Thika, aliahidi ya kwamba idara ya Afya ya umma ingeendesha shughuli ya kupuliza dawa ili kuangamiza corona.

“Janga hilo limeshika kila mmoja na kwa hivyo ni lazima tushikane kwa pamoja ili tuliangamize,” alisema Dkt Nyoro.

Alisema ameweka mikakati kabambe kuhusu jinsi ya kukabiliana na janga la corona.

Alisema tayari ameweka mikakati katika hospitali tofauti Kiambu, zitakazojipanga vilivyo kukabiliana na homa hiyo.

Maafisa wa Afya ya umma walizuru maeneo tofauti wakitekeleza shughuli hiyo katika mji wa Thika.

Walinyunyiza dawa katika vituo vya magari na hata matatu zilizokuwa katika steji.

Kutoka hapo walipuliza dawa kwa pikipiki za bodaboda ambapo wahudumu walirithika na hatua hiyo.

Bw John Kimani ambaye anaendesha bodaboda mjini Thika alisema hatua iliyochukuliwa na Kaunti ya Kiambu ni nzuri kwani hiyo ni njia moja ya kupunguza corona kuenea zaidi .

“Sisi kama wanabodaboda tutafuata maagizo ya serikali kuona ya kwamba tunabeba abiria waliovalia barakoa,” alisema Bw Kimani.

Wengine walionufaika ni waendeshaji wa Tuktuk ambao kwa wakati huu wameshauriwa kubeba msafiri mmoja pekee kila mmoja.

Baada ya maafisa hao kukamilisha shughuli hiyo mjini Thika, walikwenda maeneo mengine ya mashinani kutekeleza kazi hiyo.

Naibu mkurugenzi wa Afya ya umma kaunti ndogo ya Thika, Bw Samuel Mureithi, alisema baada ya kukamilisha eneo hilo la Thika maafisa wake watazuru maeneo mengine muhimu ili kupambana na janga hilo.

“Tunajaribu kuhakikisha janga hilo linapunguzwa kwa njia yoyote ile. Lakini ili tufanikiwe, ni sharti tushirikiane na kila mmoja,” alisema Bw Mureithi.

Alisema kwa muda wa wiki mbili zilizopita idara hiyo ya Afya ya umma imepuliza dawa katika masoko kadha kama Madaraka, Wangige, Ruaka, na Limuru.

Alisema wataendelea kunyunyiza dawa hiyo kwa wiki mbili zijazo ili kuona jinsi mambo yatakavyokuwa.

“Jambo muhimu kwa sasa ni kuwahimiza wananchi popote walipo wazingatie maagizo yote ya serikali ili tuweze kupambana na janga hili,” alisema Bw Mureithi.