Mjue rafiki mnafiki

Mjue rafiki mnafiki

Na BENSON MATHEKA

DOREEN alitamani sana kuolewa na Peter waanzishe familia hadi alipokutana na Susan aliyebadilisha mawazo yake alipomweleza anavyochukia ndoa na watoto pia.

Doreen alishawishika na akaanza kuchukia sio tu ndoa bali pia akamtema Peter, mwanamume aliyekuwa akimpenda kwa dhati na na alikuwa amewekeza katika mipango ya maisha yao ya baadaye.

Kile ambacho Doreen hakufahamu ni kuwa Susan alinuia kuvuruga uhusiano wake na Peter ili aweze kumnyemelea. Susan alivunja urafiki wake na Doreen na baada ya miezi minane akafunga ndoa na Peter.

“Mtu niliyedhani alikuwa rafiki wa dhati alitumia ujanja, akanipokonya mpenzi wangu kwa kunifanya nichukie ndoa. Hapo niliamini kuwa wajinga ndio waliwao,” Doreen aliambia Pambo katika kituo cha Big Hearts jijini Nairobi ambako amekuwa akipata ushauri nasaha.

Mwanadada huyu anakubaliana na washauri kwamba ni makosa kuruhusu marafiki kumfahamu au kuzoeana sana na mpenzi wako au hata kujihusisha na marafiki wanaochukia ndoa.

“Ukiruhusu marafiki wazoeane au wamfahamu sana mtu wako, unajiweka katika hatari ya kumpoteza. Ukisikia rafiki yako akizungumzia mabaya kuhusu wanaume (ikiwa wewe ni mwanamke) au wanawake (ikiwa wewe ni mwanamume), elewa kwamba anafanya hivyo kwa sababu anakuonea wivu. Anaweza kuwa anamtamani mtu wako na analenga kukushawishi umuache ili amnyakue,” asema Teddy Wanjohi, mwanasaikolojia wa kituo cha Big Hearts.

Kulingana na Seth Kerubo, mshauri wa wanandoa katika shirika la Family Resource, Nairobi, watu huwa wanavuruga mahusiano yao ya mapenzi kwa kuwasikiliza wengine ambao huwa hawana nia njema kuwahusu.

“Sisemi ni makosa kusikiliza ushauri wa mtu unayemwamini, lakini kabla ya kuchukua hatua, kuwa mjanja pia. Fanya uchunguzi wako binafsi, usiwe mtu wa kubebewa akili na kuamuliwa mambo na watu wengine,” aeleza.

Mtaalamu huyu anasema kwamba watu wamekolewa na wivu hivi kwamba wanachomea picha wenzao kwa wachumba wao hasa wakiangukia walio na uwezo wa kifedha, wanaojukumika na walio na maono.

“Ili kukinga penzi lako, usianike mipango yenu kwa marafiki.Ni muhimu pia kuelewa tabia za marafiki lakini kumbuka kuwa moyo wa mtu sio kitabu unachoweza kusoma ukurasa wa kwanza hadi wa mwisho, ni msitu unaoficha siri nyingi ambazo zinaweza kuwa hatari kwako,” asema Kerubo.

You can share this post!

Wawili wakana kuiba piki piki kuuza nchini Ethiopia

MALEZI KIDIJITALI: Wazazi wawe mfano mzuri wa vifaabebe!

T L