Mjukuu wa Moi asalimu amri, sasa kupimwa DNA

Mjukuu wa Moi asalimu amri, sasa kupimwa DNA

Na JOSEPH OPENDA

HATIMAYE mjukuu wa rais wa zamani marehemu Daniel Moi amekubali kutii agizo la mahakama la kumtaka afanyiwe uchunguzi wa DNA kuthibitisha ikiwa yeye ndiye baba mzazi wa watoto wawili wa aliyekuwa mkewe Glady Jeruto Tagi.

Mahakama ya Nakuru, Jumatano iliambiwa kwamba, Bw Collins Kibet Moi alijifikisha katika maabara ya hospitali ya Lancet mjini Nakuru Nakuru Ijumaa wiki jana kutolewa chembechembe zake za DNA.

Kibet, ambaye ni mwanawe marehemu Jonathan Toroitich, alitii agizo la mahakama baada ya uamuzi kutolewa kwamba, asukumwe jela kwa kosa la kudharau maagizo kadhaa ya mahakama.

Bi Jeruto, kupitia wakili wake David Mongeri, alithibitisha mbele ya mahakama kwamba, Bw Kibet alifika katika hospitali hiyo kulingana na agizo la mahakama.

“Tunathibitisha kuwa (Kibet) alijitokeza katika maabara Ijumaa na sampuli zake na zile za watoto hao wawili zikachukuliwa kwa uchunguzi,” akasema Bw Mongeri.

Mahakama iliambiwa kuwa, matokeo ya uchunguzi huo yatatolewa ndani ya muda wa wiki tatu.

Mnamo Julai 14, Hakimu Mkuu Benjamin Limo aliamuru mjukuu huyo wa Rais mstaafu Moi asukumwe gerezani kwa kosa la kudharau amri za mahakama.

Hata hivyo, alimwachilia huru kwa dhamana ya Sh100,000.

Bw Kibet ambaye ambaye pia ameamriwa agharamie malezi ya watoto hao, alikwepa kuhudhuria vikao vya mahakama. Hatua hiyo ilichangia mahakama kutoa amri kwamba alazimishwe kufika mbele yake.

Alipofika binafsi mahakamani, Bw Kibet aliiomba mahakama hiyo imsamehe akieleza kuwa kutofika kwake hospitalini kulichangiwa na kukatika kwa mawasiliano kati yake na mawakili wake.

Ajabu ni kwamba ni yeye, mshtakiwa, aliomba uchunguzi wa DNA ufanywe ili kubaini ikiwa ndiye baba mzazi wa watoto hao wenye umri wa miaka tisa na 11.

Katika kesi yake, Jeruto alidai Kibet alitelekeza wajibu wake wa kugharamia malezi ya watoto hao kwa kipindi cha miaka minane.

You can share this post!

EACC yalaumiwa kwa kuhujumu juhudi za kukombolewa kwa fedha...

Afisa wa polisi aliyetoweka mwaka mmoja uliopita bado...