Habari za Kitaifa

Majuto ya Mjukuu wa Moi: Collins Kibet sasa atoweka, kesi ya kuhepa malezi ikimuandama

March 22nd, 2024 1 min read

NA JOSEPH OPENDA

MJUKUU wa Rais wa Pili wa Kenya marehemu Daniel arap Moi, Collins Kibet, ametoweka, na amekwepa kufika mahakamani kwa miezi miwili, huku kesi ya kuhepa malezi ya watoto wake ikimuandama.

Mahakama ilikuwa imetoa maagizo kwake kufika mbele yake, ikimtaka kueleza sababu ambapo hafai kuadhibiwa kwa kukaidi maagizo ya kuwajibikia malezi ya watoto wake.

Licha ya juhudi kadhaa za mawakili kumkabidhi maagizo ya mahakama, hajakuwa akionekana.

Wakili Steve Biko alieleza ugumu ambao amekuwa nao kumpata Bw Kibet. Wakili hiyo anamwakilisha mke wa zamani wa Bw Kibet, Bi Gladys Cheruto.

Akiwa mbele ya Hakimu Mkuu Kipkurui Kibellion kwa njia ya mtandao, Bw Biko alisema kwamba imekuwa vigumu kumfikia Bw Kibet kupittia anwani zake katika eneo la Kabarak, Kaunti ya Nakuru na bustani ya Kabarnet, Kaunti ya Nairobi. Pia, simu yake ya rununu imezimwa tangu Januari.

“Juhudi za kumpelekea maagizo ya mahakama kupitia anwani yake ya kibinafsi hazijafaulu kwani hakuwa huko. Niliambiwa kwenda katika bustani ya Kabarnet, Nairobi, ambako pia sikumpata,” akasema Bw Biko.

Wakili huyo aliiomba mahakama kumwongeza muda wa siku saba zaidi kuendelea kumtafuta Bw Kibet, ikizingatiwa kwamba kuna njia nyingine mbadala.

Pia, alitoa pendekezo kwa mahakama kumwagiza aliyekuwa wakili wa Kibet kuieleza aliko mteja wake, kwani mshtakiwa hakuwa amembadilisha wakili wake.

Hakimu alikubali ombi la Bw Biko kumwongezea muda zaidi, akisisitiza kuhusu umuhimu wa kutilia maanani mahitaji ya watoto walio katika kesi hiyo.

Awali, mahaka ilikuwa imemwagiza Bw Kibet kufika mbele yake Februari 21 ili kujibu ombi la Bi Cheruto, kwamba mshtakiwa alikuwa akikaidi maagizo ya mahakama tangu Juni 2022.

Maagizo hayo yanamtaka Bw Kibet kutoa usidizi wa kifedha kwa watoto wake katika masuala ya elimu, matibabu na burudani.