Mjumbe wa Taliban anyimwa fursa kuhutubia kikao cha UN

Mjumbe wa Taliban anyimwa fursa kuhutubia kikao cha UN

Na AFP

MKUTANO wa Mataifa wanachama wa Umoja wa Mataifa (UNGA) ulimazilika jana, huku mwakilishi wa kundi la Taliban linaloongoza Afghanistan akizuiliwa kuhutubia kongamano.

Mwakilishi wa serikali ya Myanmar pia alinyimwa fursa ya kuhutubia viongozi wa nchi 100 walipokutana jijini New York, Amerika, kufuatia utata wa kisiasa katika nchi hiyo.

Mwakilishi wa Afghanistan katika Umoja wa Mataifa (UN), Ghulam Isaczai, aliratibiwa kuhutubia kongamano la UNGA kabla ya kufungwa baadaye jana.

Lakini kundi la Taliban lilimwandikia barua Katibu Mkuu wa UN, Antonio Guterres, likitaka Isaczai asiruhusiwe kuhutubu likishikilia kuwa halimtambui.Kundi la Taliban lilisema kwamba Isaczai aliteuliwa na Rais Ashraf Ghani aliyeng’olewa mamlakani mwezi uliopita, ‘hivyo kazi yake iliisha’.

Badala yake, kundi hilo lilimtaka Guterres kuruhusu waziri wa mashauri ya kigeni wa serikali ya Taliban, Amir Khan Muttaqi, aruhusiwe kuhutubia UNGA.

Kamati kuu ya UNGA inayojumuisha mataifa ya Amerika, China na Urusi iliahidi kufanya mkutano wa dharura kujadili ombi hilo la Taliban.

Mkutano huo wa kamati, hata hivyo, haukufanyika.Baadaye, maafisa wa UN walisema kuwa ombi hilo la Taliban lilichelewa na wakaruhusu Isaczai kuhutubia kongamano.Isaczai alitumia fursa hiyo kusihi UN kuongeza vikwazo dhidi ya serikali ya Taliban.

Mwakilishi wa Myanmar katika Umoja wa Mataifa, Kyaw Moe Tun, alizuiliwa kuhutubu kwa sababu nchi yake inakumbwa na msukosuko wa kisiasa.

Tun aliteuliwa na Rais Aung San Suu Kyi, aliyeng’olewa mamlakani kupitia mapinduzi ya kijeshi mnamo Februari, mwaka huu.Mnamo Mei, mwaka huu, wanajeshi waliteua jenerali wa jeshi wa zamani, lakini UN haijaidhinisha uteuzi wake.

Mwakilishi wa Guinea katika UN, Aly Diane, aliruhusiwa kuhutubia kongamano. Diane aliteuliwa na Alpha Conde aliyepinduliwa mapema mwezi huu na kundi la wanajeshi. Serikali ya jeshi inayoongozwa na Kanali Mamady Doumbouya, haikutuma mwakilishi wake katika kongamano la UNGA.

Shirika la Maendeleo la Mataifa ya Afrika Magharibi (Ecowas) tayari limewekea Guinea vikwazo huku likitaka wanajeshi wakabidhi mamlaka kwa utawala wa kiraia.

Hiyo ilikuwa mara ya kwanza kwa viongozi wa nchi mbalimbali kukutana ana kwa ana tangu kutokea kwa mlipuko wa virusi vya corona duniani.

Viongozi wa nchi kadhaa, akiwemo Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya na mwenzake wa Ufaransa Emmanuel Macron, walihutubia kongamano hilo kwa njia ya video.

Miongoni mwa viongozi waliohudhuria kongamano hilo na kupata fursa ya kuhutubu ni Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania na kiongozi mpya wa Zambia Hakainde Hichilema.

You can share this post!

Wakulima wa chai kulipwa bonasi ya juu mwaka ujao

CCM yakataa kuingia UDA