Habari Mseto

Mkaguzi mkuu wa matumizi ya pesa za serikali akosoa mpango wa KQ kusimamia JKIA

March 23rd, 2019 2 min read

Na CHARLES WASONGA

MKAGUZI Mkuu wa Matumizi ya Pesa Serikalini, Edward Ouko ameelezea tashwishi aliyo nayo kuhusu mpango wa kuwezesha Shirika la Ndege Nchini (KQ) kusimamia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA), akisema mpango huo umegubikwa na siri.

Kwenye ripoti iliyowasilishwa katika Bunge la Kitaifa wiki hii na kiranja wa wengi Benjamin Washiali Bw Ouko anasema afisi yake haikupewa stakabadhi muhimu kuhusu mpango huo unaojulikana kwa Kimombo kama ‘Privately Initiated Investment Proposal (PIIP)’.

Japo taarifa ya Uwaziri (cabinet memo) ilitayarishwa na kuwasilishwa mbele ya baraza la mawaziri mnamo Mei 29, 2018, kuhusu mpango huo, Bw Ouko anasema kuwa hamna ushahidi kwamba usimamizi wa Mamlaka ya Kusimamia Viwanja vya Ndege Nchini (KAA), ambayo husimamia viwanja vyote vya ndege nchini, ikiwemo JKIA, ilihusishwa katika mpango huo.

“Hatujapewa ripoti ya uchunguzi wa awali, kuhusu mpango huo, ambao ungejadiliwa katika baraza la mawaziri,” Bw Ouko akasema.

Hayo yanajiri wakati ambapo Katibu wa Wizara ya Uchukuzi Esther Koimett alisema kuwa taarifa ya uwaziri ilikuwa imasaka uidhinishaji kuhusu hatua ambazo Kenya inafaa kuchukua kuimarisha ufanisi wa safari za anga Afrika.

“Hii itawezekana tu kwa kuimrishwa kwa uwanja wa ndege wa JKIA kuweza kuwa kivutio kikuu,” akasema Bi Koimett.

Taarifa ya uwaziri iliwasilishwa na Waziri wa Fedha Henry Rotich pia haiwasilishwa kwa afisi ya Bw Ouko kwa ukaguzi sawa na barua kutoka wa Mkuu wa utumishi wa umma Joseph Kinyua.

Stakabadhi hizo pia hazikuwasilishwa kwa KQ na KAA kwa ukaguzi wao na maafikiano kuhusu mpango huo.

Ripoti ya Ouko ilichochewa na kamati ya bunge kuhusu uwekezaji (PIC) ambayo ilikumbana na mpango huo ilipokuwa ikikagua matumizi ya fedha ya KAA.

Ukaguzi maalumu

Hii ilimlazimu mwenyekiti wa kamati hiyo Abdulswamad Nassir kumwomba Bw Ouko kufanya ukaguzi maalumu kuhusu mpango huo ili kubaini ikiwa inaweza kufaulu na ni mpango wa kuwafaidi walipa ushuru.

Katika mapendekezo yake ya awali, PIC ilipendekeza kusitishwa kwa mpango huo hadi pale mkaguzi wa matumizi ya fedha za serikali atakapowasilisha ripoti yake.

Hii ina maana kuwa sasa PIC itaweza kuwaita maafisa wahusika kufika mbele yake kuuliza ni kwa nini stakabadhi muhimu hazikuwasilishwa ili yakaguliwe na kubaini lengo la mpango huo.

Spika Justin Muturi aliitaka PIC kuendelea na uchunguzi wake kuhusu mpango huo na kuwasilisha ripoti yake bungeni.

Kibarua kama hicho pia aliipa kamati ya bunge kuhusu uchukuzi lakini ikijikite katika masuala ya sera, wafanyakazi, uzingativu wa sheria na utaratibu, faidi kwa jamii na taifa na masuala mengine yanayohusu jamii.