Habari Mseto

Mkakati mpya wa kupunguza ada ya umeme

May 17th, 2018 1 min read

Na BERNARDINE MUTANU

Ni habari njema kwa Wakenya baada ya serikali kuondoa baadhi ya ada inazotoza umeme.

Hatua hiyo ni kumaanisha gharama ya matumizi ya umeme itapungua kwa kiwango fulani. Kwa sasa, asilimia 77 ya malipo ya stima huenda kwa ushuru.

Ada hizo ni asilimia 24.8 isiyobadilika, asilimia 27.7 ya uzalishaji wa umeme ambapo asilimia 13.6 ni ushuru wa matumizi ya umeme(VAT), sarafu ya kigeni ni asilimia nane na asilimia tatu ni mfumko wa bei ambapo Mamlaka ya Kusimamia Rasilimali ya Maji (WARMA) hupokea asilimia o.1.

Zinazobakia ndio umeme ulionunuliwa na mteja, alisema mkurugenzi wa ERC Pavel Oimeke hivi majuzi.

Lakini Rais Uhuru Kenyatta aliagiza baadhi ya ada hizo kuondolewa. Kutokana na hilo, Waziri wa Fedha na mwenzake wa Kawi Charles Keter watakutana kujadiliana agizo hilo.

Ada zinazolengwa ni ile ya WARMA na ERC. Lakini ada hizo ni asilimia 0.001 ya bili yote ya stima.

Ada nyingine inayotarajiwa kuondolewa ni ile ya stima maeneo ya mashambani ambayo ni asilimia tano ya kiwango cha umeme kilichonunuliwa.

Wakenya sasa watalipa Sh10 chini kwa kila 50 kWh kutoka Sh24.03. Hatua hiyo ilichukuliwa baada ya Wakenya kulalamikia kiwango cha juu cha gharama ya umeme.