Habari za Kitaifa

Mkanganyiko ilani ya serikali ya kuahirisha kufungua shule ikiwasili kuchelewa

April 29th, 2024 2 min read

NA WAANDISHI WETU

HALI ya suitafahamu ilishuhudiwa baada ya mamia ya wanafunzi wa shule za msingi na sekondari kuhudhuria shule saa kadhaa baada ya serikali kuahirisha tarehe ya kufunguliwa kwa shule.

Shule ziliratibiwa kufunguliwa Aprili 29, 2024 lakini sasa zitafunguliwa Mei 6, 2024 baada ya serikali kurefusha likizo kwa wiki moja.

Wazazi waliopigwa na butwaa walisema hawakujua kalenda ya shule imebadilishwa.

Katika vituo tofauti vya mabasi Mombasa, Kilifi na Kwale, wanafunzi walionekana wakirejea shuleni.

“Ninafanya kazi na kuishi Mombasa na ilibidi nimpeleke mtoto shuleni Kilifi mapema lakini niligundua baadaye kuwa kuna mabadiliko,” alisikitika Bi Messaid Omar akisema angemtuma mtu shuleni kumrejesha mtoto wake nyumbani.

Baadhi ya wanafunzi walikuwa tayari wamefika shuleni Jumapili jioni katika baadhi ya shule kaunti ya Taita Taveta.

Wanafunzi wawili waliosafiri kutoka Kiambu hadi Shule ya Upili ya Shimo la Tewa Mombasa walitumiwa nauli na wazazi wao warudi tena nyumbani.

Katika Kaunti ya Siaya, uchunguzi wa Taifa Leo katika vituo vya mabasi umeonyesha wanafunzi walikata tiketi za basi kusafiri Jumatatu hasaa wanaosomea nje ya kaunti.

“Nimelazimika kuuza tiketi ya basi kwa abiria mwingine anayesafiri leo,” alisema Bw Martin Otieno aliyemlipia nauli binti yake.

Kwingineko katika kaunti ya Kisii, wanafunzi waliorejea shuleni walitumwa nyumbani baada ya kalenda ya shule kubadilishwa ghafla.

“Serikali inafaa kuwajibika. Huwezi kutoa taarifa kuhusu kuahirishwa kwa ufunguzi wa shule usiku wa manane,” aliteta mzazi Edgar Omwando.

Wanafunzi wengine waliohudhuria shule kaunti za Nakuru, Nyandarua na Samburu walipigwa na butwaa kukuta madarasa na ofisi za shule bila wanafunzi na walimu.

Watoto hawa walionekana wakitembea mijini wasijue la kufanya.

“Nilitoka nyumbani saa kumi na moja asubuhi kwenda Nairobi. Sikujua kulikuwa na mabadiliko,” alisema mwanafunzi Benson Maina akihangaika mjini Nyahururu.

Hali ilikuwa sawia katika shule za upili za Bahati Girls, Nakuru Boys, na Nakuru Girls wanafunzi wakichanganyikiwa.

Mambo yalikuwa yayo hayo kaunti ya Vihiga. Zaidi ya wanafunzi 20 wa Shule ya Upili ya Bunyore walipigwa na butwaa kugundua tarehe ya ufunguzi wa shule imebadilishwa.

“Tumeweka mikakati kuwahifadhi wanafunzi ambao wamerejea shuleni kwa juma moja zaidi,” alifichua Mwalimu Mkuu Judith Agade.

Kaunti ya Kisumu pia haikusazwa. Kuna wanafunzi waliofunga safari kwenda Shule ya Upili ya Arya wakakuta malango yamefungwa.

“Nilipokea habari kwa kuchelewa baada ya kumpeleka mtoto shuleni na ilibidi nimrejeshe mtoto wangu nyumbani,” alisema Bi Isabela Amondi.

Haya yanajiri baada ya Waziri wa Elimu Ezekiel Machogu kutoa taarifa usiku wa manane kuwa kalenda ya shule imebadilika ili kutahadhari na athari ya mafuriko.

“Ripoti zilizotufikia, na ambazo zimethibitishwa na vitengo vingine vya serikali zinaonyesha kwamba shule mbali mbali zimeathiriwa vibaya na mafuriko,” ilisema taarifa hiyo.

Kwa hivyo serikali ililazimika kuahirisha ufunguzi wa shule kwa Muhula wa Pili hadi Mei 6, 2024.

Taarifa ya Winnie Atieno, Lucy Mkanyika, Kevin Mutai, Maureen Ongala, Kassim Adinasi, Wycliffe Nyaberi, Waikwa Maina, John Njoroge, Victor Raballa na  Geoffrey Ondieki

Tafsiri: Labaan Shabaan