Jamvi La Siasa

Mkanyagano ODM kuhusu viti vilivyobaki wazi


MZOZO mkali unanukia ndani ya ODM, wajumbe wakitofautiana kuhusu maeneo yanayostahili kupokezwa viti vilivyosalia wazi baada ya viongozi wanne wa chama hicho kuteuliwa kuwa mawaziri.

Wajumbe sasa wanataka viti hivyo visambazwe kwa usawa ili kusawiri ODM kama chama chenye sura ya kitaifa.

Magavana wa zamani Hassan Joho (Mombasa), Wycliffe Oparanya (Kakamega) ambao walikuwa manaibu kiongozi wa chama, waliteuliwa mawaziri katika Serikali Jumuishi.

Vivyo hivyo, Mwenyekiti wa ODM John Mbadi na mbunge wa Ugunja, Opiyo Wandayi ambaye alikuwa msimamizi wa masuala ya kisiasa, sasa watahudumu kama mawaziri iwapo wataidhinishwa na bunge.

Kusambazwa kwa vyeo hivyo sasa kumefanya Kinara wa Upinzani Raila Odinga aanze kujikuna kichwa, wandani wake kutoka Luo Nyanza wakionekana kuvitaka viti vyote.

Hatua hiyo imeonekana kuzua mgawanyiko, viongozi kutoka jamii ya Abagusii wakitaka wapewe cheo kimoja cha naibu kiongozi wa chama baada ya kukosa kupokezwa wadhifa wa uwaziri na mrengo wa Upinzani.

Wiki jana, viongozi kutoka eneo la Gusii waliandika barua ya malalamishi kwa Bw Odinga, wakisema kuwa eneo hilo linahisi kutengwa ilhali limekuwa likiunga mkono ODM kwa miaka mingi.

Viongozi hao ni Gavana wa Kisii Simba Arati, Seneta wa Nyamira Okong’o Omogeni na wabunge Clive Gisairo (Kitutu Masaba), Patrick Osero (Borabu), Irene Mayaka (mteule), Anthony Kibagendi (Kitutu Chache Kusini) na Obadiah Barongo (Bomachoge Borabu), pamoja na Mwekahazina wa ODM Timothy Bosire.

Bw Kibagendi na Mbunge wa Nyaribari Masaba Daniel Manduku walikuwa wanaumezea mate wadhifa wa kiongozi wa wachache ambao ushapokezwa Junet Mohamed.

Mbunge wa Suba Kaskazini Millie Odhiambo naye ashapokezwa wadhifa wa Kiranja wa Wachache.

Viongozi kutoka ukanda wa Nyanza na Magharibi sasa wanaonekana kugawanyika kuhusu nani anastahili kuwa naibu kiongozi wa chama hicho.

Gavana wa Homa Bay, Gladys Wanga na mwenzake wa Kisii, wote wanataka wadhifa huo.

Mnamo Jumapili, zaidi ya wenyekiti 21 wa ODM kutoka kaunti mbalimbali walimuidhinisha Bw Arati kuwa naibu wa Bw Raila wakisema ana maono ya kuongoza chama.

“Tumeafikiana kuhusu mwelekeo ambao chama kinastahili kuchukua. Tunamuidhinisha Gavana Arati achukue wadhifa wa naibu kiongozi wa chama,” akasema Mwenyekiti wa ODM, Kaunti ya Narok, Bw Kazo Roho Torome.

Mwenyekiti wa vuguvugu la wanawake ndani ya ODM, Kaunti ya Trans Nzoia, Bi Dorothy Aduba naye alisema Bw Arati ameonyesha ukakamavu na uaminifu kwa Raila kwa hivyo huu ni wakati wa kumtuza.

Aliungwa mkono na Mwenyekiti wa ODM, Kaunti ya Nakuru Benard Miruku na viongozi wengine wa chama kutoka Bonde la Ufa.

Hapo jana, kundi la wabunge wanawake wa ODM walimuunga Bi Wanga kuwa naibu kiongozi wa chama. Kwa upande mwingine, mbunge wa Likuyani Innocent Mugabe naye anataka Gavana wa Kakamega Fernandes Barasa awe naibu kiongozi wa ODM.