Habari

MKASA WA ETHIOPIA: Dhiki ya kuzika mchanga

March 18th, 2019 2 min read

NA MASHIRIKA

SHIRIKA la ndege la Ethiopia limewapatia jamaa wa familia za watu 157 waliokufa kwenye ajali wiki iliyopita, mifuko yenye mchanga kwenda kuzika. Hii ni baada ya mabaki ya walioangamia kukosekana.

Shirika la habari la BBC lilinukuu shirika la AP Jumapili likiripoti kuwa kila familia ilipewa kilo moja ya mchanga uliochukuliwa kutoka eneo ambapo ndege hiyo ilianguka, ilipokuwa ikielekea Nairobi kutoka mji mkuu wa Ethiopia, Addis Ababa.

Hii ilifanyika huku idadi ya Wakenya waliokufa ikiongezeka kutoka 32 hadi 36, baada ya kufahamika kuwa wanne zaidi walikuwa wametumia paspoti za mataifa ya kigeni kusafiri.

Hapo jana, mmoja wa familia ya Cosmas Rogony, ambaye ni miongoni mwa walioangamia, aliambia Taifa Leo kuwa jamaa wao waliokuwa wamesafiri Addis Ababa walirejea wakiwa na mchanga waliopewa Ethiopia.

Alisema kuwa wazee wa ukoo wa marehemu watafanya kikao leo kuamua kitakachofanyika baada ya mwili wa mpendwa wao kukosekana.

BBC ilisema kuwa Ethiopian Airlines ililazimika kuwapa mchanga jamaa wa waliokufa baada ya kuwa vigumu kutambua miili.

Familia zimeambiwa kuwa itachukua hadi miezi sita kutambua mabaki ya miili ya 157 walioangamia.

Wachunguzi wamekusanya vipande vidogo vidogo takriban elfu tano vya mabaki ya miili ya binadamu katika eneo la ajali. Vipande hivyo ni kama vile vidole na mifupa. Ripoti zinasema sehemu kubwa zaidi ya mwili ambayo ilipatikana ni mkono.

Haijafahamika kiini cha ajali hiyo kufikia sasa huku uchunguzi unaoshirikisha Ethiopia, Ufaransa na Amerika ukiendelea.

Hapo jana, maelfu ya waombolezaji walilazimika kufanya ibada ya wafu mbele za majeneza yaliyokuwa tupu baada ya kukosa miili ya wapendwa wao.

Majeneza 17 yalifunikwa kwa bendera ya kitaifa ya Ethiopia na kuzungushwa katika barabara za Addis Ababa, huku baadhi ya jamaa za marehemu wakizimia.

Wasafiri kutoka mataifa zaidi ya 30 walikuwa kwenye ndege hiyo ilipoanguka katika eneo la Bishoftu, kilomita 60 kutoka Addis Ababa.

“Upelelezi wa kisa kikubwa namna hii huhitaji uchanganuzi wa kina na muda mrefu kufahamu ukweli,” akasema Waziri wa Uchukuzi wa Ethiopia, Dagmawit Moges.

Vifaa vya kurekodi shughuli za ndege almaarufu kama ‘black box’ vilipatikana na kupelekwa Ufaransa ili habari zilizomo zitolewe na kuchunguzwa.

Wapelelezi nchini Ufaransa walisema Jumamosi kuwa walifanikiwa kutoa habari zilizokuwemo kwenye vyombo hivyo na kuzikabidhi kwa wapelelezi wa Ethiopia.

Ilikuwa imefichuka awali kwamba rubani wa ndege hiyo aliwasiliana na kituo kikuu cha uwanja wa ndege wa Bole, na akaeleza alikuwa anakumbwa na matatizo kudhibiti ndege. Aliruhusiwa kurejea uwanjani humo lakini ndege ikaanguka kabla arudi.

Idara ya Uchukuzi wa Ndege Amerika, ilisema uchunguzi wake kuhusu mienendo ya ndege hiyo umeonyesha dakika zake za mwisho zilifanana na zile za ndege ya Lion Air, ambayo ilianguka Indonesia mnamo Oktoba mwaka uliopita na watu 189 wakafariki.

Ndege zote mbili zilikuwa aina ya Boeing 737 MAX 8, ambazo sasa zimepigwa marufuku kusafiri katika mataifa mengi ulimwenguni ikiwemo Amerika, ambako ndege hizo hutengenezwa.