HabariSiasa

Mkasa wa Likoni: Serikali yaomba Wakenya msamaha

October 3rd, 2019 2 min read

Na CHARLES WASONGA

SERIKALI kupitia Wizara ya Uchukuzi imewaomba Wakenya msamaha kwa kuchelewa kuanzisha shughuli za kuokoa mama na bintiye ambao walikufa maji Jumapili katika kivuko cha Likoni.

Pia, serikali imedinda kuelekeza kidole cha lawama kwa Shirika la Feri Nchini (KFS) kwa kukosa kutekeleza wajibu wake kwa makini kuwahakikishia usalama watumiaji wa feri zake katika kivuko hicho.

Waziri Msaidizi wa Uchukuzi na Miundo Msingi Chris Obure Alhamisi aliwaambia wabunge kwamba ingawa kisa hicho ni cha kusikitisha, “hatua fulani za tahadhari na usalama zilipasa kuzingatiwa.”

“Najua taifa linaomboleza kufuatia vifo vya Wakenya hao wawili ambavyo vingeepukwa. Tunaomba msamaha kwa familia iliyopoteza wapendwa wao na Wakenya huku tukituma risala zetu kwa familia hiyo,” Bw Obure akaambia wanachama wa Kamati ya Bunge la Kitaifa kuhusu Uchukuzi alipofika mbele yao katika majengo ya Bunge, Nairobi.

“Rasilimali zote pamoja na vifaa vimetolewa kwa ajili ya kufanikisha kutolewa kwa miili ya wawili hao,” akaongeza.

Zaidi ya saa 120 baada ya mkasa huo kutokea, familia ya Mariam Kigenda, 35, na bintiye mwenye umri wa miaka minne Amanda Mutheu imekuwa ikisubiri kutolewa kwa miili yao.

Mnamo Jumapili Bi Kigenda na bintiye ambaye ni mwanafunzi katika Shule ya Msingi ya MM Shah Academy walikufa maji baada ya gari lao aina ya Toyota ISIS, lenye nambari ya usajili KCB 289C lililobebwa na feri ya MV Harambee iliteleza na kutumbukia baharini katika kivuko hicho chenye shughuli nyingi.

“Ikiwa kanuni za kimsingi kuhusu usalama zingefuatwa, ajali iliyotokea Jumapili ingeepukwa,” Bw Obure aliwaambia wanachama wa kamati hiyo wakiongozwa na mwenyekiti wao David Pkosing (Mbunge wa Pokot Kusini).

Waziri huyo Msaidizi aliahidi kuwa wizara yake itachukua hatua zifaazo za kuimarisha usalama katika feri zote zinazomilikiwa na Shirika la Feri Nchini (KFS).

Hata hivyo, wanachama wa kamati hiyo; Gideon Mulyungi (Mwingi ya Kati), Tom Odege (Nyatike) David Kiaraho (Ol-Kalou) na Shadrack Mose (Kitutu Masaba) walisisitiza kuwa wazara hiyo inafaa iwajibikie ajali hiyo au iwachukulie hatua za kinidhamu wasimamizi wa shirika hilo.

“Inakuwaje kwamba gari hilo lilielea majini kwa dakika 10 na hakuna hatua yoyote iliyochukulia kulitoa?” Bw Mulyungi akasema.

Akaendelea: “Msimamo wangu ni kwamba mkurugenzi mkuu wa KFS Bakari Gowa anapasa kupigwa kalamu ili Mkenya mwingine ambaye anaweza kutulinda baharini.”

Naye Bw Mose akauliza: “Mwanamume huyo (Bw Gowa) alijibu maswali bila umakini nilipomtizama kwenye runinga. Mbona usalama hautiliwi maanani katika feri zetu?