Habari Mseto

Mkasa wa Solai: KHRC yalaumu taasisi za serikali

May 29th, 2018 1 min read

Na FRANCIS MUREITHI

TUME ya kutetea haki za kibinadamu (KHRC) imelaumu taasisi za serikali kwa kupuuza dalili za mapema kabla ya kutokea kwa janga la mauti la bwawa la Solai.

Kulingana na tume hiyo Mamlaka ya kitaifa ya mazingira nchini(NEMA) na Mamlaka ya usimamizi wa rasilimali ya maji (WARMA) zinafaa kulaumiwa kutokana na kutepetea kazini.

“WARMA, NEMA na Kampuni ya kahawa ya Patel zinafaa kufanyiwa uchunguzi na iwapo zitapatikana zilitepetea kazini basi zinafaa kukabiliwa kisheria,” ikasema taarifa ya tume iliyotolewa mjini Nakuru wikendi iliyopita.

Mkurugenzi mkuu wa tume hiyo George Kegoro alisema mipasuko kwenye kuta za bwawa hilo ililalamikiwa na wenyeji lakini hakuna hatua iliyochukuliwa.

“Wananchi walikuwa wameibua maswali kuhusu hali ya bwawa hilo kuvuja mwaka 2016 lakini hakuna kilichofanyika kukabili hali hiyo.

Hakuna bwawa katika mashamba ya Patel lililokuwa na leseni ya kudumu na inashangaza kwamba NEMA haikujua uwepo wa mabwawa hayo hadi janga hili lilipotokea,” akasema Bw Kegoro.

Bw Kegoro aliongeza kwamba kisa kama hicho kilitokea katika eneo hilo mwaka wa 2012 wakati bwawa jingine lilipovuja maji lakini hakuna maafa wala uharibifu uliotokea.

Wakati huo huo tume hiyo imeitaka serikali ya kaunti ya Nakuru, Serikali kuu na Mmiliki wa shamba la kahawa la Patel kuzisaidia familia zilizoathirika kwa kupoteza mali yao kando na kujenga miundo msingi kama daraja na shule zilizoharibika.

Pia wamelitaka Shirika la msalaba mwekundu  kusaidia katika kuwatambua na kuwalipa fidia wananchi walioathrika kisha imewapa wamiliki wa ardhi kwenye shamba la Nyakinyua hati miliki zao za ardhi.